ASILIMIA 58 kati ya 100 ya watoto chini ya miezi sita nchini ndio wanaonyonya maziwa ya mama.
Hivyo wazazi wa watoto asilimia 42 wanaobaki wanatakiwa nao kunyonyesha watoto maziwa yao huku wakichukua tahadhari ya ugonjwa wa Covid-19.
Kauli hiyo ilitolewa na Ofisa Utafiti Mwandamizi Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Ruth Mkopi wakati akizungumza namna bora ya wanawake kunyonyesha huku wakiwalinda watoto katika kipindi hiki ambacho dunia nzima inapambana na ugonjwa wa Covid-19.
Mtalaamu huyo alisema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi sasa hakuna ushahidi wa kiutafiti unaoeleza uwepo wa maambukizi ya virusi vya corona toka kwa mama kwenda kwa mtoto kipindi cha ujauzito au kupitia maziwa ya mama wakati wa unyonyeshaji.
"Nipende kuwasihi wanawake wanaonyonyesha watoto wadogo katika kipindi hiki tunachoendelea kujikinga na corona, naomba mwendelee kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na wataalamu ili muweze kuwalinda watoto wenu,"alisema Mkopi.
Aidha aliwashauri wazazi wa watoto hao kuendelea kulinda afya za watoto chini ya miezi sita kwa kuepuka kuwapa maziwa ya makopo yanayouzwa madukani kwa uzushi kuwa yanaondoa maradhi kwa mtoto jambo ambalo sio sahihi.