Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nguo za ndani za kubana zatajwa kusababisha ugumba kwa wanaume

11435 Nguo+pic TanzaniaWeb

Sun, 12 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wanaume wanaopenda kuvaa suruali au nguo za ndani za kubana hawana budi kuchukua tahadhari.

Tahadhari hiyo inakuja baada ya utafiti mpya kubaini kuwa nguo za ndani za kubana husababisha ugumba kwa wanaume.

Utafiti huo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya cha Havard, Uingereza na kuchapishwa katika Jarida la Afya ya Uzazi la T.H Chan umebaini kuwa nguo hizo ni moja ya sababu za ugumba.

Profesa Jorge Chavaro aliyesimamia utafiti huo alisema walizifanyia utafiti sampuli za mbegu za kiume kutoka kwa wanaume 656.

Alisema wanaume hao walichaguliwa kutoka kliniki ya matibabu ya wenye matatizo ya uzazi katika Hospitali ya Massachusetts kati ya mwaka 2000 na 2017.

Wanaume waliofanyiwa utafiti huo waliulizwa maswali mbalimbali ikiwamo ni aina gani ya nguo za ndani wanazopenda kuvaa.

Daktari huyo alilinganisha wanaume wanaovaa nguo za ndani zinazobana na ambao wanavaa zinazoacha nafasi.

“Tuligundua kuwa wanaovaa nguo za ndani zenye nafasi, mbegu zao za kiume zina uwezo mkubwa wa kutungisha mimba na nyingi ukilinganisha na wale wanaovaa nguo za ndani za kubana,” alisema Dk Chavarro.

“Wanachotakiwa kufanya ni kubadilisha aina nguo za ndani kwa mwanamume kama tahadhari kwa sababu kuvaa nguo za kupwaya ni kitu rahisi sana ni kitendo tu cha wao kwenda kununua nguo mpya za ndani,” alisema Dk Chavarro.

Jarida la Afya la Lancet linasema ubora wa mbegu za wanaume ni pamoja na kuishi katika joto la kadri, kati ya nyuzi 36 hadi 37.

Kuwa na kichwa kilichochongoka, mkia uliochongoka na kuwa na maji ya kadri ya kuziwezesha kusafiri kwa hadi kwenye nyumba ya uzazi.

“Sifa hizi ndizo zinazoiwezesha mbegu kutungisha mimba,” inaeleza ripoti ya Lancet.

Dk Chavarro aliongeza: “Kwa kawaida mwanamume anayeishi maeneo ya joto anapaswa kuwa makini sana, ili kuhifadhi vizuri mbegu zake anatakiwa kutumia mavazi yenye kupitisha hewa siyo yenye kubana.”

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya (Muhas), Dk Peter Wangwe alisema kuna ukweli, kwenye suala hilo.

“Ni kwa sababu ya joto kali na jinsi maumbile ya mwanamume yalivyo, via vyake vya uzazi vimewekwa hapo ili visipate joto zaidi ya lile la kawaida, hivyo anapovaa nguo za kubana anaongeza joto,” alisema.

Dk Wangwe ambaye pia ni mtaalamu wa afya ya uzazi alisema joto la mwili kwa kawaida ni nyuzi 36.7 hadi 37 hivyo mwanamume anapovaa nguo za kubana joto huongezeka na kuharibu mbegu za kiume.

“Pale ndipo ambapo mbegu za kiume huzalishwa, hivyo joto linapozidi, mbegu hizo hufa kabla ya muda wake,” alisema.

Alitaja sababu nyingine ya nguo hizo kusababisha ugumba kwamba korodani zinapobanwa, damu inayotoka pale haisambazwi ipasavyo mwilini hivyo hubaki na kuzalisha majimaji ambayo huharibu ubora wa mbegu.

“Hali hii ikizidi huweza pia kusababisha mabusha,” alisema.

Alisema wanawake hawaathiriwi na uvaaji wa nguo za kubana kwa sababu mayai yao yapo tumboni na wanaume mayai yapo nje ya mwili.

Utafiti uliofanywa na daktari wa masuala ya afya ya uzazi, Henry Mwakyoma wa Muhas mwaka 2010, ulibaini kuwa kati ya wanaume 221 waliofanyiwa utafiti, asilimia 30.03 walikuwa na mbegu dhaifu. Pia ulibaini kuwa asilimia 17.2 walikuwa hawana kabisa mbegu zenye uwezo wa kutungisha mimba.

Dk Mwakyoma alisema utafiti huo ulifanikiwa baada ya wanaume wengi kuanza kujitokeza kupima kama ni wagumba au la.

“Hata kama mwanamume aliwahi kuwa na mtoto huko nyuma, nasisitiza kuwa anaweza akapata tatizo hilo sasa kulingana na mazingira,” alisema.

Pamoja na joto kwenye korodani, Dk Mwakyoma alitaja sababu nyingine kuwa ni unene kupita kiasi, sababu za kimazingira kama kufanya kazi migodini na maeneo yenye kemikali.

UTILITI

• 656 wanaume waliofanyiwa utafiti Uingereza

• 221 wanaume waliofanyiwa utafiti Tanzania

• 30 asilimia ya wanaume ambao mbegu zao zilikuwa dhaifu na haziwezi kutungisha mimba

Chanzo: mwananchi.co.tz