Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngozi za ng’ombe, nguruwe kutumika matibabu ya moyo

Aliyepandikizwa Moyo Wa Nguruwe Afariki Dunia Ngozi za ng’ombe, nguruwe kutumika matibabu ya moyo

Fri, 15 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwa mara ya kwanza wagonjwa wenye tatizo la kuziba kwa mshipa mkubwa wa damu ndani ya moyo wameanza kutibiwa kwa njia ya tundu dogo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)

Kupitia teknolojia hiyo mpya ambayo kifaa maalumu huingizwa hadi kwenye mshipa husika na kuweka valvu inayotengenezwa kwa ngozi ya ng’ombe au nguruwe, tayari wagonjwa watatu wamekwishatibiwa.

Awali, wagonjwa waliobainika kuwa na maradhi hayo ya moyo, walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu, sasa huduma hiyo itaendelea kutolewa lakini itawahusu vijana pekee.

Akielezea teknolojia hiyo, Daktari bingwa wa matibabu kwa njia ya tundu dogo JKCI, Khuzeima Khunbhui alisema huduma hiyo itawanufaisha watu wenye umri wa kuanzia miaka 70 na kuendelea.

"Kipindi cha nyuma tulifanya upasuaji kufungua kifua na kuweka valvu kwenye mshipa wa moyo (kwa wagonjwa wote, wakiwemo wa miaka 70 na kuendelea), lakini sasa tutatumia njia ya tundu dogo kuweka valvu hiyo kwenye mshipa wa moyo ulioziba.

“Valvu hii inayotengenezwa kwa kutumia ngozi ya ng’ombe au nguruwe, ina uwezo wa kudumu kwa miaka 15 kwenye mshipa wa moyo,” alisema daktari bingwa huyo.

Alisema utafiti unaendelea duniani kuangalia kama valvu zinazowekwa sasa zinaweza kudumu zaidi ya miaka 15, endapo vijana watawekewa.

Alifafanua kuwa, tiba wanayopata vijana wenye matatizo hayo ni kuwekewa chuma ndani ya mshipa wa moyo, ambacho kinadumu kwa muda mrefu huku mgonjwa akitakiwa kutumia dawa kwa maisha yake yote. Alisema kama vijana watatibiwa kwa njia ya tundu dogo, itawahitaji kufanyiwa mabadiliko ya valvu watakayowekewa kila baada ya miaka 15.

Ushuhuda mgonjwa

Donald Lema wa Machame, Kilimanjaro akisimulia namna alivyobaini ugonjwa huo, alisema kujisikia mwili kukosa nguvu na akitembea mita 100 lazima apumzike, hivyo alikwenda kufanya uchunguzi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC na kuambiwa valvu moja ya moyo ililegea,

“Niliambiwa matibabu ni India au JKCI, nilikuja JKCI na nimepatiwa matibabu na sasa naendelea vizuri, sikusikia maumivu eneo lolote la mwili,” alisema.

Alisema gharama ya matibabu alipaswa kulipa Sh80 milioni lakini alilipa Sh25 milioni, kiasi kingine kiligharamiwa na Serikali.

Kiini cha tatizo

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo JKCI, Tatizo Waane alisema ugonjwa huo hutokana mabadiliko ya mwili. Alielezakwa watu wazima tatizo hilo huchangiwa na umri mkubwa ambapo valvu husababisha kuzalishwa kwa madini chokaa ndani ya mshipa wa moyo.

“Chokaa hizo hujikusanya na baadaye hufanya damu kushindwa kutoka na kuingia kwenye moyo, hivyo figo, ubongo na viungo vingine mwilini huanza kupata damu kidogo na hivyo mhusika huanza kupata maumivu ya kichwa na kifua,” alisema.

Dk Waane alisema kupitia njia ya tundu dogo, daktari humhudumia mgonjwa ndani ya saa moja hadi mbili na mgonjwa kuondoka wodini siku inayofuata, tofauti na upasuaji ambao mgonjwa hutumia zaidi ya wiki wodini.

Kuhusu gharama ya matibabu alisema, mgonjwa mmoja hapa nchini sasa atatibiwa kwa Sh80 milioni tofauti na nje ya nchi ambapo mgonjwa anatibiwa kwa Sh150 milioni.

Uwezo wa watalaamu JKCI

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge alisema uwezo wa wataalamu ndani ya taasisi hiyo uliwezeshwa na wenzao wa Hospitali ya Starcare ya India.

Alisema madaktari wa JKCI kwa asilimia 90 wana uwezo wa kutoa huduma hiyo.

Alisema JKCI imeendelea kuwa kituo cha utalii tiba na wagonjwa kutoka nchi 20 za Afrika zinazofika kwenye taasisi hiyo kupokea matibabu.

Kutokana na wigi wa wagonjwa, Dk Kisenge aliiomba Serikali iipatie jengo lingine kwa ajili ya kuwahamishia wagonjwa, ombi ambalo Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk John Jingu alisema linafanyiwa kazi.

Dk Jingu alisema uwekezaji kwenye sekta ya afya una umuhimu mkubwa, akifafanua kuwa kwa mwaka huu Serikali imeweka Sh7 trilioni kwenye sekta ya afya.

Kwa upande wa wataalamu, alisema zaidi ya Sh10.9 bilioni zimewekezwa na Serikali kusomesha wataalamu kwenye nchi mbalimbali, ambao watakuja kutoa matibabu ya kibingwa nchini. Kati Julai na Desemba mwaka huu, alisema JKCI imehudumia zaidi ya wagonjwa 3,000 na kuingiza Sh920 bilioni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live