Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndugu wa wagonjwa Hospitali ya Ligula watakiwa kuwa na vitambulisho

52830 Pic+wagonjwa

Wed, 17 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Baada ya uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Ligula, kuanzisha utaratibu wa vitambulisho kwa ndugu wanaohudumia wagonjwa, wananchi wamepongeza hatua hiyo.

 Baadhi ya ndugu wa wagonjwa ambao hawakutaka kutajwa, wamepongeza hatua iliyochukuliwa na uongozi kwamba siku za nyuma baadhi ya watu walikuwa wakijihusisha na vitendo vya ngono kwenye mazingira ya hospitali hiyo.

“Watu walikuwa wanajilalia hospitali na eneo lilivyo kubwa wengine walikuwa wanatongozana hapahapa na kumalizana ndani ya eneo hili (hospitali), lakini mwingine anataka tu na yeye aje ashindwe na mgonjwa kwa sababu anajua ataletewa chakula,” amesema mmoja wa watoa taarifa.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Aprili 17, 2019  baadhi ya ndugu hao wamedai utaratibu umebadilika na msaidizi wa mgonjwa analazimika kuwa na kitambulisho maalumu wakati wote hospitalini hapo.

Mmoja wa ndugu wa mgonjwa, Rabia Namkame amesema ametokea wilayani Masasi alifika hospitalini hapo kumuona binti yake mjamzito lakini walinzi walimtoa nje.

“Hatuna sehemu ya kupikia wala kulala, ilhali tunatoka mbali na huko ndani wanahitaji kitambulisho hapa (nje ya geti) tunafukuzwa muda wowote tutafute pakulala na mvua kama hizi tutaenda wapi?” amehoji Namkame.

Naye ndugu mwingine, Mwajuma Salum amesema alifika hospitalini hapo juzi usiku baada ya mama yake kung’atwa na nyoka, baada ya kupatiwa huduma yeye  alitakiwa kuondoka.

“Nashukuru hawakumnyanyasa mama yangu amehudumiwa kawaida na kunikopesha dawa nikapewa kiasi ninachotakiwa kulipa, lakini nashangaa nimekaa ndani usiku wote asubuhi naambiwa nitoke nje na mguu wake umevimba hawezi kutembea, leo ndio nakuja kuambiwa habari za kitambulisho,” amesema Mwajuma.

Katibu wa afya hospitalini hapo, Dk Tereven Invocaviths amesema wameweka utaratibu wa vitambulisho ili kumwezesha ndugu wa mgonjwa kuingia ndani baada ya kufanyika tathmini kuona kama anahitajika kubaki.

Amesema kabla ya utaratibu huo ilifika wakati mgonjwa mmoja anakuwa na ndugu 15 na wote wanataka kukaa hospitalini, hivyo kumnyima mgonjwa na daktari uhuru wa kumhudumia lakini pia kuhatarisha afya zao.

“Utaratibu wa vitambulisho ni baada ya mgonjwa kufanyiwa tathmini pamoja na ndugu kufanyiwa tathmini iwapo umetoka mbali, au anahitajika kuendelea kukaa na mgonjwa na kama huhitajiki maana yake unatakiwa ufike eneo la hospitali muda tu wa kuangalia wagonjwa tofauti na hapo hautatakiwa kuwapo eneo la hospitali,” amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz