Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nchi za EAC zilivyojizatiti kuzalisha chanjo ya corona

A320dbbae87818395c5b3f1f5136f3cd.jpeg Nchi za EAC zilivyojizatiti kuzalisha chanjo ya corona

Tue, 6 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

NCHI za Jumuiya Afrika Mashariki (EAC) zinaweka mikakati ya kila nchi kutengeneza chanjo yake ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Kufanikiwa kwa nchi hizo kupata chanjo kunaelezwa kutasaidia kwa kiasi kikubwa kukabili maambukizi ya virusi hivyo kwa ufanisi na gharama ndogo.

RWANDA

Wiki hii Rwanda imetia saini makubaliano ya Faranga bilioni 3.6 na Umoja wa Ulaya (EU) ili kuwezesha uwekezaji katika kutengeneza chanjo.

Taarifa ya Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB) ilieleza kuwa, makubaliano hayo yanalenga kuimarisha uwezo wa Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Rwanda (FDA) kutengeneza chanjo.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame hivi karibuni alisema serikali yake ipo katika maandalizi ya mwisho kujenga kiwanda cha kutengeneza chanjo za magonjwa mbalimbali ikiwamo dhidi ya corona.

Alisema kwa kushirikiana na wadau wengine wa kimataifa, maandalizi ya kujenga kiwanda hicho yamefika hatua kubwa.

"Tumeshirikiana na viwanda ambavyo vina teknolojia ya juu maarufu kama MRNA, hii ni teknolojia mpya na ya kisasa ambayo hutumia njia mbalimbali kutengeneza chanjo za kuzuia hata magonjwa mengine, lakini pia tunazungumza na wadau katika masuala ya fedha na hapa tunasema huenda miezi michache ijayo mtasikia taarifa nzuri," alisema.

Rwanda imetangazwa kama moja ya vituo vya utengenezaji wa chanjo barani Afrika, baada ya Nigeria na Afrika Kusini.

UGANDA

Uganda imeeleza kuwa chanjo inayotengenezwa nchini humo ipo katika hatua za mwisho kukamilika.

Rais Yoweri Museveni alisema hivi karibuni kuwa, chanjo ya nchi hiyo itakuwa bora kuliko nyingine kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na virusi vya aina mbalimbali.

“Aprili tulikuwa na wagonjwa wachache, lakini sasa kuna wagonjwa wengi watakaowezesha kufanya majaribio,” alisema Rais Museveni na kuongeza kuwa, kufikia mwakani, Uganda haitakuwa tegemezi kwa watu wa nje katika suluhisho la matibabu.

''Tuna wanasayansi wetu ambao wanajua dawa za jadi. Mmoja wao anafahamu mimea inayotumika kutibu maambukizo ya virusi, aliponya wagonjwa wapatao 30 kwa kutumia mimea,” alisema.

TANZANIA

Nchini Tanzania, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi alisema wizara hiyo imeimarisha mpango wa tatu wa kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 kwa kuanza mkakati wa kujenga kiwanda cha kutengeneza chanjo ya corona nchini ambacho kwa makadirio ya awali kitagharimu Sh bilioni 80.

Alisema tayari wameanza mchakato wa kutengeneza chanjo ya virusi hivyo nchini ili kupunguza gharama ya kuagiza nje ya nchi na kuzifanya ziwe karibu na wananchi.

Alisema: "Wataalamu tunao wengi na kiwanda hicho hakitatengeneza chanjo ya Covid pekee, hata ugonjwa huo ukiisha tutaendelea kuzalisha chanjo nchini."

Chanzo: www.habarileo.co.tz