Wananchi wa wilaya ya Namtumbo wameishukuru serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma za upasuaji kwa akina mama wajawazito wanaopata changamoto za kujifungua, huduma ambayo imeanza miezi sita iliyopita.
Wananchi hao wameeleza kuwa awali, huduma za upasuaji kwa ajili ya uzazi zilikuwa zikifanywa na kituo kimoja tu cha Afya cha Namtumbo, ambacho kilikuwa kinatumika kama hospitali ya Wilaya kabla ya hospitali mpya ya Wilaya kuanza kutoa huduma hizo.
Hatua hii ni juhudi za serikali kuimarisha huduma za uzazi pingamizi wa mama na mtoto kwa kusambaza vifaa vya upasuaji na utunzaji wa watoto wanaohitaji uangalizi maalumu wakati wa kujifungua(CEmONC)
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt. Aaron Hyera ameeleza kuwa, kutoka mkoa wa Ruvuma, wilaya ya Namtumbo ilikuwa inaongoza kupeleka wazazi wenye changamoto hospitali ya mkoa, kutokana na kuwa na kituo kimoja tu kilichokuwa na huduma za upasuaji, hivyo kwa huduma hiyo kupatikana kwenye vituo viwili wilayani hapo kutasaidia sana.
Mbali na huduma ya upasuaji,serikali imeiwezesha hospitali ya Wilaya ya Namtumbo mashine za X-ray na Ultrasound, na kuanza kutoa huduma hizo mpya kwa wananchi wa Namtumbo huduma waliyokuwa wakiifuata mkoani Ruvuma.
Dkt. Hyera ameeleza kuwa wananchi wa kijiji cha mbali zaidi kiitwacho Likusanguse wilayani humo walilazimika kwenda umbali wa kilometa 310 kufuata huduma za X-ray.
Wilaya ya Namtumbo ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 49 ikiwa ni pamoja na zahanati 43, vituo vya afya vitano (5) na hospitali ya Wilaya moja (1).
Vifaa hivyo vimesambazwa na kusimikwa na Wizara ya Afya kupitia Bohari ya Dawa (MSD) katika mpango wa maboresho ya hospitalo za Wilaya nchoni pamoja na vituo vya kutolea huduma za afya nchini vilivyoongezewa hadhi.