Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namna ya kukuza ufahamu kwa mtoto mchanga

48687 Cristian+Bwaya

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nimefanya utafiti kutazama namna walimu na wazazi wanavyowasaidia watoto wao kukuza uelewa wa mambo. Nimefuatilia malezi na kazi za shule zinazotolewa kwa watoto wa madarasa ya awali, shule za msingi na sekondari.

Nimejifunza jambo moja kubwa. Kwamba kazi nyingi wanazopewa watoto hazilingani na umri wao na hivyo haziwasaidii kujenga uelewa wao wa mambo.

Katika mfululizo wa makala hizi, nitajaribu kuainisha uwezo wa mtoto kiufahamu na kutoa mapendekezo ya namna mzazi au mwalimu anavyoweza kukuza ufahamu wa mtoto. Makala haya yanaanza na umri wa mtoto mchanga, kuanzia siku moja mpaka mwaka mmoja. Makala yanayofuata yataangazia umri wa kati ya mwaka mmoja na miaka miwili, kisha miaka mitatu mpaka miaka sita. Mwisho nitaangazia mtoto wa miaka saba mpaka kumi na miwili.

Pamoja na tafiti nyingi zilizofanywa kuainisha uwezo wa mtoto mchanga kiakili, kazi za mwanasaikolojia nguli wa Uswisi, Jean Piaget ndizo zinazotumika zaidi kutusaidia kuelewa uwezo wa kiakili wa mtoto mchanga. Kwa mujibu wa Piaget, ukuaji wa ubongo wa mtoto mchanga unategemea mambo mawili makubwa.

Kwanza, kile ambacho milango ya fahamu ya mtoto inakipokea. Taarifa zinazofikia ubongo wa mtoto kupitia macho, masikio, ngozi, ulimi na pua ndizo hasa zinazosaidia kuimarisha au kudumaza uwezo wake kiufahamu. Maana yake ni kwamba mtoto anayepokea taarifa nyingi zaidi ndiye anayechangamshwa kiakili zaidi kuliko mwenzake anayepokea taarifa chache au asiyepokea kabisa.

Ushauri kwa wazazi na walezi wa watoto wa umri huu ni kuhakikisha milango ya hisia inachangamshwa kadri inavyowezekana. Hakikisha mtoto amezungukwa na vifaa vyenye rangi mbalimbali kumvutia mtoto. Nguo anazovaa, kuta za mahali anapokaa, vifaa anavyochezea mtoto, inashauriwa viwe na rangi za kung’aa kupata uzingativu wa mtoto. Rangi tofauti tofauti anazoona mtoto zinaongeza udadisi kwenye ufahamu wa mtoto, hali ambayo kwa kawaida, hukuza uwezo wa kuchakata taarifa kadri anavyokua.

Lakini pia, inashauriwa kuzungumza na mtoto. Hata kama mtoto hajapata uwezo wa kuongea, bado masikio yake yanasikia. Sauti yako ni muhimu katika kutengeneza tajiriba inayokuza ufahamu wa mtoto.

Sambamba na kuzungumza na mtoto, tunashauriwa kumkumbatia kadri inavyowezekana. Hisia za kuguswa, tafiti zimebaini, mbali na kujenga uhusiano wa karibu na mtoto, zinasisimua ukuaji wa ufahamu wake. Katika utafiti mmoja, uwezo wa kiakili wa watoto waliojengewa mazoea ya kukumbatiwa na walezi wao ulilinganishwa na uwezo wa watoto wengine waliokosa ukaribu huo kwa wazazi wao. Matokeo yalionyesha kuwa wale waliokumbatiwa walikuwa na uwezo mzuri kiakili kuliko wale, ambao kwa sababu moja au nyingine walikosa kukumbatiwa. Tafsiri yake ni kwamba kukumbatiwa kunachangia kukuza uelewa wa mtoto.



Chanzo: mwananchi.co.tz