Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namna ya kuboresha maisha ya mtoto mwenye VVU

90127 VVU+PIC Namna ya kuboresha maisha ya mtoto mwenye VVU

Sat, 28 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati mwezi huu uliokuwa na maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ukielekea ukingoni, ni lazima kuboresha maisha ya mtoto anayezaliwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU).

Kwa kawaida watoto wanaweza kupata maambukizi kutoka kwa mama kabla ya kuzaliwa, wakati na baada ya kuzaliwa au kunyonyesha.

Kuna mambo mzazi au mlezi akiyafanya kwa mtoto aliyezaliwa VVU husaidia kuboresha maisha kwa upande wa kimwili na kiakili.

Mambo hayo humsaidia mtoto mwenye VVU kuepukana na matatizo mbalimbali ya kiafya yatokanayo na magonjwa sugu na nyemelezi.

Zingatia ushauri na matibabu

Mzazi au mlezi anashauriwa kupata ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu wa afya wenye mafunzo maalumu ya VVU ili kukabiliana na tatizo hilo.

Vile vile kupata elimu hiyo ndiyo husaidia kuitumia kulinda afya ya mtotoaliyeambukizwa VVU.

Kama mtoto mwenye VVU alishaanza matibabu ya dawa za kufubaza makali ya virusi (ARVs), ni lazima dawa hizi apewe maisha yake yote.

Dawa hizi ni muhimu kwa kuwa ndizo zinazomwongezea muda wakuishi na kadiri anavyotumia ndivyo kinga ya mwili inavyoongezeka hatimaye afya ya mwili kuimarika.

Ushauri nasaha na kufahamu umuhimu wa dawa za ARVs pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa matibabu ya mtoto husaidia kumjengea imani na dawa hizo tangu akiwa mtoto mpaka ukubwani.

Kumjenga kitabia mapema kuna faida kubwa kwa kuwa husababisha kushikamana na matibabu na kumfanya asiache kutumia dawa hata akiwa mkubwa.

Pale, unapoona viashiria na dalili za magonjwa yoyote ni vizuri kumpeleka katika huduma za afya mapema kwa kuwa ni rahisi kulikabili tatizo katika hatua za awali.

Ikumbukwe kuwa watoto wenye VVU wapo katika hatari zaidi ya kushambuliwa na maradhi ikilinganisha na wasio na VVU.

Mlo kamili

Vyakula mchanganyiko yaani wanga, protini, mafuta, mboga za majani na matunda na unywaji wa maji ya kutosha ni muhimu kwa mtoto.

Vyakula hivi ndivyo vinavyoupa mwili nguvu na joto, kujenga mwili na kinga ya mwili.

Mlo kamili haimanishi ni mlo wenye gharama kubwa bali ni vyakula ambavyo vipo katika jamii yetu na vinapatikana kwa urahisi sana.

Mfano wa vyakula hivyo ni mboga mboga kama mchicha, matembele na karot.

Vyakula vya protini ni kama maharagwe ya soya, kunde, njegere, mazao ya mifugo na majini.

Kwa upande wa matunda ni pamoja na maembe, machungwa na matikiti maji.

Hivyo ni muhimu mzazi au mlezi kulima bustani za mboga na matunda na si vibaya kufuga kuku wakienyeji kwa ajili ya mayai na nyama.

Mboga mboga, matunda na protini ni muhimu katika ujenzi wa kinga ya mwili.

Ikumbukwe kuwa mtoto mwenye VVU ni rahisi kushambuliwa na maradhi kwa kuwa kinga inakuwa dhaifu.

Pia, itahitajika mtoto huyo kupata mapumziko ya kutosha zaidi ya saa nane. Hiyo husaidia kinga ya mwili kuimarika.

Kwa watoto wenye umri wa miaka miwili ni vyema kuhakikisha wanaendelea michezo ya kitoto na wenzake humfanya kuwa na mwili imara na kuwa mwenye furaha.

Kumjenga kisaikolojia

Hili linaanzia kwa mzazi kwamba lazima akubaliane na hali halisi baada ya kuelewa ushauri aliopewa kutoka kwa wataalamu wa afya.

Ni jukumu lake kumjenga kisaikolojia mtoto huyo, inahitajika kumkuza vizuri kwa kumuonyesha upendo na furaha. Mfanye asijione yuko tofauti, pale atakapofikia umri wakuanza kutambua ni vizuri akawa anaelimishwa na mambo mbalimbali yaliyo na tija na afya yake.

Baadaye ataelimika na kukubaliana na hali yake pasipo kumpa msongo wa mawazo au kupata sonona. Uwapo wa mambo haya mawili huweza kumfanya asiwe mwenye afya njema kutokana na kuumia kihisia.

Kumpa elimu na malezi bora

Watoto wenye VVU nao wanahitaji malezi bora kuanzia kwa wazazi au walezi mwishowe na jamii kiujumla. Watoto hawa wanahitajika kulelewa kwa kuelekezwa na kufundishwa mambo mema na mazuri. Pia, wajengwe kitabia kwa kuzungumza nao na kuwaelekeza pasipo adhabu.

Vizuri kufahamu kuwa watoto hawa wana udhaifu mkubwa kihisia ukilinganisha na watoto wengine, mfano watoto wenye VVU ni rahisi kupata huzuni haraka au kupata hasira kali. Haki ya kupata elimu kwa watoto hawa huwa ni lazima kama watoto wengine.

Pale itakapofikia muda wa kuanza shule ni muhimu kuanzishwa shule za awali.

Habari nzuri ni kuwa tayari kuna sheria zinazowalinda watoto hawa kwa baadhi ya nchi.

Mtengenezee mazingira bora ya kuishi

Pale unapokuwa umemwekea mazingira bora ya ndani na nje ya nyumba vizuri humfanya mtoto ajihisi mwenye utulivu wa kimwili na kiakili.

Watoto hawa huwa ni rahisi kupatwa na huzuni au shinikizo la kiakili.

Ni vyema kuweka wazi tatizo la mtoto wako kwa watu wakaribu kama vile ndugu jamaa na marafiki, katika hatua za awali.

Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu

Chanzo: mwananchi.co.tz