Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nafasi 16 madaktari bingwa zakosa waombaji

Doctorrrrrrr Nafasi 16 madaktari bingwa zakosa waombaji

Fri, 1 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wizara ya Afya imewapangia vituo vya kazi watumishi 1,605 huku ikisema nafasi 16 za madaktari bingwa hazikupata waombaji.

Kukosekana kwa waombaji hao kunakuja ikiwa ni siku chache baada ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutangaza kuwa nafasi 736 zimekosa waombaji wenye sifa.

Waziri wa Tamisemi, Innocent Bashungwa alizitaja kada hizo ni daktari wa meno nafasi (50), tabibu meno (43), tabibu msaidizi (244), mteknolojia mionzi (86) na muuguzi ngazi ya cheti (313).

Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Abel Makubi leo Julai Mosi, 2022 nafasi hizo ni kati ya nafasi ya ajira 1,621 za kada ya afya zilizotangazwa na wizara hiyo.

Amesema kada ambazo zilinufaika na nafasi hizo ni madaktari, wafamasia, wateknolojia wa dawa, wateknolojia wa maabara, wateknolojia wa mionzi, wateknolojia wa macho.

Kada nyingine ni maofisa uuguzi, watoa tiba kwa vitendo, wazoeza viungo kwa vitendo, maofisa afya mazingira pamoja na wasaidizi wa afya.

Amesema baada ya kupokea kibali cha ajira, wizara ilitangaza nafasi 1621 za kada za afya kupitia katika tovuti yake kuanzaia Aprili 16 hadi 29,2022.

Hata hivyo, Profesa Makubi amesema kutokana na umuhimu wa zoezi hilo wizara iliongeza muda hadi Mei 3, 2022 ambapo ndio ilikuwa siku ya kufungwa kwa mfumo.

Amesema hadi kufungwa kwa tangazo hilo kulikuwa na waombaji 19,464 waliokamilisha taratibu za uombaji kwenye mfumo na waombaji 8404 hawakukamilisha taratibu za uombaji.

“Kati ya waombaji 19,464 waliofanyiwa uchambuzi waombaji 7,897 walikidhi vigezo vya awali…Hatua iliyofuatiwa na uchambuzi wa kina na jumla ya waombaji 1,605 walichaguliwa,”amesema Profesa Makubi.

Amesema nafasi 16 za madaktari bingwa hazikupata waombaji hivyo nafasi hizo zitajazwa kwa mujibu wa kanuni na sheria za ajira katika utumishi wa umma.

Profesa Makubi amesema waajiriwa hao wamegawanywa katika hospitali za rufaa za mikoa ambapo wamepata watumishi 1063, hosptali za kanda (200), vituo vya afya (118), vituo vya damu salama (38), hospitali maalumu (90) na vituo vya mipakani (96).

Amezitaja baadhi ya sababu za waombaji wengine kukosa ajira ni kutojaza kabisa au kutojaza kikamilifu namba za usajili zilizotolewa na mabaraza yao, hivyo kusababisha kushindwa kutotambuliwa.

“Baadhi ya waombaji kufanya makosa ya kutumia namba za usajili za wanataaluma wengine wanaotambulika na baraza au kutumia namba za mtahiniwa zilizotumika wakati wa mitihani ya baraza au chuo,”amesema.

Amesema sababu nyingine ni waombaji kuomba nafasi za ajira ambazo hawana sifa nazo ambapo ametoa mfano wa muombaji mwenye sifa ya stashahada kuomba nafasi ya shahada na wengine kutokidhi vigezo vya muundo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live