Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NMB YATENGA BILIONI 2/- KUENDELEZA ELIMU, AFYA

F588c0d293e41726b32ed5d728b525cc.jpeg NMB YATENGA BILIONI 2/- KUENDELEZA ELIMU, AFYA

Sun, 15 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BENKI ya NMB imetenga zaidi ya Sh bilioni mbili mwaka huu wa fedha kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu na afya nchini ikiwa ni utekelezaji wa sera ya kurejesha sehemu ya faida kwa jamii.

Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, alisema kiasi hicho ambacho ni ongezeko mara dufu ya bajeti ya mwaka wa fedha ulioisha, kinadhihirisha dhamira ya benki hiyo yenye matawi mengi zaidi nchini, kufanya uwekezaji endelevu na wenye tija katika sekta hizo muhimu.

Kwa mujibu wa Meneja huyo wa kanda wa benki, mwaka jana ilitengwa Sh bilioni moja.

Katika jitihada hizo, juzi benki hiyo ilitoa msaada wa vifaa vya ujenzi na madawati vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 72.5 kwa shule za umma na vituo vya afya katika wilaya za Bunda Mkoa wa Mara, Kaliua mkoani Tabora na Kinondoni mkoani Dar es Salaam. Akizungumza wakati wa kupokea misaada yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 50 kwa shule za msingi na vituo vya huduma ya afya wilayani Kinondoni, Mkuu wa Wilaya hiyo, Godwin Gondwe alisema uwekezaji unaofanywa na NMB katika sekta za elimu na afya una tija kwa jamii kwa sababu unasaidia Taifa kuondokana na maadui ujinga na maradhi.

“Inachofanya NMB kupitia Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ni zaidi ya uwekezaji kwa Taifa na watu wake. Kupitia programu hii, Taifa linakuwa na kizazi chenye afya bora, wasomi bora, viongozi, wafanyakazi na wafanyabiashara bora,” alisema Gondwe.

Awali akikabidhi misaada hiyo iliyotolewa kwa Hospitali ya Mwananyamala, Kituo cha Afya Bunju, shule mbili za msingi na nne za Sekondari wilayani Kinondoni, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Richard alisema misaada iliyotolewa ni utekelezaji wa sera ya kurejesha kwa jamii asilimia moja ya faida ya benki kila mwaka.

Wakati Hospitali ya Mwananyamala na Kituo cha Afya Bunju vikikabidhiwa misaada ya vitanda vyenye thamani ya Sh milioni 14 , shule za Msingi Mikumi na Wazo Hill ya Wazo zilipokea misaada ya mabati 50 na madawati 100, wakati shule za sekondari Kigogo, Mzimuni, Boko Mtambani na Kiseuke zimepewa jumla ya viti 250 na meza 250, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh36.6 milioni.

Kwa upande wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Meneja wa NMB kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus alikabidhi misaada ya mabati 400 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 13.5 kwa shule za sekondari za Manyamanya na Nyanaguta ambapo kila shule imepokea mabati 200.

Akipokea misaada hiyo Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Nassari alishukuru NMB kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku akiwasihi wazazi na walezi wilayani humo kujitolea kwa hali na mali kuunga mkono juhudi hizo kwa kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika shule za maeneo yao.

“Sitakuwa na urafiki na wazazi, walezi na viongozi wa vijiji na kata ambazo shule zake hazina vyumba vya kutosha vya madarasa, matundu ya vyoo, maabara na mabweni kwa ajili ya watoto wetu. Kila mmoja katika eneo lake aonyeshe juhudi na serikali pamoja na wadau wengine wakiwemo NMB wataunga mkono,” alisema Nassari.

Kwa wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, NMB imetoa msaada wa mabati 90 yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni tisa kwa shule za msingi Ilege na Mkiligi.

Misaada hiyo ilikabidhiwa na meneja wa NMB kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus kwa Mkuu wa Wikaya ya Kaliua, Chacha Matiko aliyeishukuru benki hiyo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu katika shule za umma.

Chanzo: www.habarileo.co.tz