Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NIMRCAF suluhisho kwa mafua makali, kikohozi kikavu

1a6af01526d788aba0c0cfd4e3d8f117 NIMRCAF suluhisho kwa mafua makali, kikohozi kikavu

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

DAWA ya NIMRCAF inayotengenezwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) inatokana na vitu mbalimbali ikiwemo pilipili kichaa, tangawizi, kitunguu swaumu, kitunguu maji chekundu na limao.

Vitu hivi vyote kila kimoja kina umuhimu wake kwenye mwili wa binadamu ikiwemo kutibu, kukinga na kuongeza kinga ya mwili. Katika hali ya maisha ya kawaida si watu wengi wanapenda kutumia vyakula vyenye ukali au uchachu kama vile pilipili, limao na ndimu, lakini kwenye dawa ya NIMRCAF, mtumiaji hana budi kuvitumia kwa ajili ya ama kuongeza kinga ya mwili au kujitibu ugonjwa au magonjwa mbalimbali ambayo dawa hii inayatibu.

Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Yunus Mgaya anaeleza umuhimu na kazi ya pilipili kichaa iliyowekwa kwenye dawa hii kwa ajili ya matumizi ya binadamu wasio na changamoto ya vidonda vya tumbo vikali.

Profesa Mgaya anasema kuwa pilipili haikuwekwa kwenye dawa hii kwa bahati mbaya bali ina kemikali ambayo ina kazi maalumu mwilini. Anasema pilipili ina kemikali inayoitwa ‘Capsaicin’ ambayo kazi yake mwilini ni kulegeza kifua kilichobana, kikohozi kikavu, kuponya tumbo linalouma, kuua bakteria, kusaidia kufanya mishipa ya damu itanuke, inazuia damu kuganda pamoja na kuimarisha kinga ya mwili.

Dawa hii ilikuwa na inaendelea kuwa msaada hata kwa watu wenye changamoto ya dalili za ugonjwa wa Covid-19 ambapo moja ya dalili za ugonjwa huo ni kupumua kwa shida kutokana na kubana mbavu na kikohozi kikavu. Huu ndiyo umuhimu na kazi ya pilipili kwenye dawa ya NIMRCAF.

Anasema pamoja na umuhimu huu wa pilipili, watu wenye matatizo ya vidonda vya tumbo vya kawaida wanaweza kuitumia lakini kwa tahadhari na wale wenye vidonda vya tumbo vikali hawatakiwa kuitumia kutokana na athari wanazoweza kupata.

“Tunaendelea na utafiti ili tuone kama tunaweza kupata dawa inayoweza kutumiwa na watu wote hata wenye vidonda vya tumbo kwa sababu pilipili haikuwekwa kwenye dawa hii kwa bahati mbaya bali ina kemikali ambayo ina kazi maalumu mwilini ambapo ukiiondoa pilipili unatakiwa utafute mbadala wake, sasa hili ni suala la utafiti,”anaeleza Profesa Mgaya.

Kutokana na umuhimu wa dawa hii, amewataka Watanzania waendelee kuitumia kwa kuwa NIMRCAF mbali na kuwa dawa, pia ni chakula katika kuimarisha kinga ya mwili.

Soko kubwa la dawa hii kwa sasa ni Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza japo mipango ya baadaye ya NIMR ni kuhakikisha inapatikana kwenye mikoa yote nchini kwa gharama nafuu.

“Unajua mahitaji ya NIMRCAF ni makubwa na sisi uzalishaji wetu unaendelea vizuri, wananchi wasiwe na wasiwasi na wala wasinunue kwa hofu kwamba hazipatikani, dawa zipo za kutosha kwenye duka letu pale Ubungo External Dar es Salaam lakini pia inapatikana kwenye mikoa ya Dodoma na Mwanza,” anasema Profesa Mgaya.

Anasema pamoja na kuwepo mahitaji makubwa ya dawa hii, pia wanatambua kuwa kuna walanguzi wanaonunua dawa hiyo kwa wingi na kuuza kwa bei ya juu.

Anasema kwa kuwa NIMR inauza dawa hii bila kuangalia sura bali kwa kuzingatia uhitaji wa mtu, hivyo inawezekana kuna watu wanaoweka msukumo kidogo kwenye upatikanaji wake japo kwa upande wao wanaendelea kuongeza uzalishaji.

“Sababu inayowafanya watu kununua dawa hii kwa hofu ni uzushi kwa sababu kuna watu wanataka kutengeneza pesa, kuna baadhi ya maduka ya dawa nimepita nimekuta wanauza dawa zetu kwa shilingi 20,000 hadi shilingi 30,000 wakati sisi tunauza shilingi 10,000.

“Mwaka jana tulisema mtu akinunua dawa hii kwetu kwa shilingi 10,000 asiende kuuza zaidi ya shilingi 15,000, lakini kwa kuwa sisi siyo mamlaka ya udhibiti hatuwezi kufanya chochote kwa kuwa ni biashara huria, ila naamini uzalishaji utakapokuwa umeimarika, bei itakuwa ya kawaida,” anaeleza Profesa Mgaya.

Amesema japo si rahisi kwa sasa kusema mahitaji yameongezeka kwa kiasi gani, amewataka wananchi kutokuwa na hofu kwa kuwa NIMR inaendelea kuzalisha dawa hizi na wanaweza kuzipata kwenye maduka ya NIMR, pia wasinunue kwa hofu kutokana na uvumi wa kuwepo kwa ugonjwa Covid-19.

Wakizungumza kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) katika kipindi kilichohusu Tiba Asili katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, Profesa Mgaya, Mkurugenzi wa Utafiti NIMR Dk Paul Kazyoba na Katibu Mkuu wa Tiba Asili, Bonaventura Mwalongo, wamewasisitiza Watanzania kuthamini vitu vyao zikiwemo dawa za tiba asili.

Dk Kazyoba anasema tiba asili ni taaluma ambayo ipo tangu kuumbwa kwa mwanadamu na isitoshe asilimia 98 ya mimea duniani haishambuliwa na virusi ambao ni chanzo cha magonjwa mengi ya mlipuko ikilinganishwa na yale yanayosababishwa na bakteria.

Amesema mimea ina uwezo wa kuzalisha kemikali tofauti tofauti kwa wingi na kufanya tiba asili kuwa fursa kubwa katika kupambana na magonjwa ya mlipuko.

“Nawaomba Watanzania tuthamini vitu vyetu kwa kuwa matatizo ni mwalimu kama ilivyokuwa kwa mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 mwaka jana, pia natoa wito kwa Wataalamu wa tiba asili waliosajiliwa na Baraza la Tiba Asili nchini kuzingatia kutoa huduma kwanza kwa wananchi badala ya kufanya biashara, naamini ndani ya miezi 24 ijayo, muonekano wa tiba asili utakuwa bora sana kuliko ulivyo sasa,” anasema Dk Kazyoba.

Katibu Mkuu wa Tiba Asili nchini, Bonaventura Mwalongo anasema matumizi ya tiba asili yamewekewa sheria tangu utawala wa Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, lakini katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, tiba asili imepata msukumo mpya hasa pale aliposisitiza matumizi ya dawa za asili katika kukabiliana na Covid-19.

“Mwaka 1979 mataifa yaliyoendelea yalikuja Afrika kuchukua mimea dawa tani 28,000 na mwaka 1980 Japan ilikuja kuchukua mimea tiba tani 22,000, kwa hiyo kinachotakiwa sasa ni kusimamia mwongozo ili kukabiliana na wadanganyifu katika tiba asili kwa kuwatambua wataalamu wote wa tiba asili,” amesisitiza Mwalongo.

Kutokana na umuhimu wa tiba asili, NIMR imewaelekeza watumiaji wa dawa ya NIMRCAF kunywa vijiko vikubwa viwili vya chakula kila baada ya saa nane kwa siku saba baada ya kuifungua kama inavyoelekezwa kwenye chupa ya dawa hiyo, pia ihifadhiwe sehemu kavu yenye joto chini ya nyuzi 30 na iwekwe mbali na watoto.

Chanzo: habarileo.co.tz