Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NIMR yatakiwa kutafiti zaidi magonjwa ya milipuko

0352d239d5655f24933721c4a1ea1d3b.jpeg NIMR yatakiwa kutafiti zaidi magonjwa ya milipuko

Thu, 26 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imeitaka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kuendelea kufanya tafiti za magonjwa ya milipuko yanapojitokeza ili kudhibiti athari zake kwa jamii.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela wakati sherehe za maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo zilizofanyika jijini hapa juzi.

Shigela aliitaka taasisi hiyo kufanya jitihada za kutafiti magonjwa pale yanapojitokeza sehemu nyingine katika dunia kabla hayafika nchini ili kuwalinda wananchi kutokana na athari zake.

“NIMR niwapongeze mlifanya kazi kubwa wakati wa corona hali iliyompa nguvu Rais John Magufuli kutangaza kuwa ugonjwa huo tumeweza kuudhibiti, hivyo endeleeni na juhudi hizo kwani mmebeba mustakabali wa taifa hili,” alibainisha Shigela.

Aidha, alisema wakati huu ambao taasisi hiyo inatimiza miaka 40, kwa kiasi kikubwa imetoa mchango mkubwa katika sekta ya afya nchini.

“Mmekuwa ni sehemu ya vielelezo vya namna ambavyo taifa hili linavyoweza kujitegemea katika utatifi na vipimo vya sampuli bila ya kutegemea wahisani kutoka nje kuja kufanya shughuli hiyo,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk Mercy Chiduo alitaja mafanikio makubwa yaliyofikiwa kutokana na utafiti wa ugonjwa wa malaria hadi kusaidia kubadilishwa kwa tiba kutoka kwenye dawa moja hadi mseto.

“Kutokana na tafiti katika ugonjwa wa malaria tumeweza kupunguza vifo kwa watoto chini ya umri wa miaka 14 ikiwemo kudhibiti maambukizi na kuboresha kinga zao dhidi ya ugonjwa huo,” alisema Dk Chiduo.

Aidha, aliiomba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutenga bajeti kwa ajili ya taasisi hiyo ijitegemee katika kufanya tafiti zake badala ya kutegemea wahisani.

Daktari mstaafu wa taasisi hiyo, Dk Acleus Rutta alisema licha ya NIMR kufanya kazi kubwa ya kudhibiti na kuratibu tafiti zote nchini zenye tija, ipo haja kwa serikali kuanza uwekezaji kwenye tafiti.

“Serikali iweke fedha kwenye tafiti badala ya kuendelea kutegemea watafiti kwani itasaidia NIMR kuweza kufanya kazi za utafiti kwa urahisi bila ya kusuasua,” alisema Dk Rutta.

Chanzo: habarileo.co.tz