Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NIMR yatakiwa kulinda tafiti zake

00839531f7399f0866ef0f6c2c38ce91.jpeg NIMR yatakiwa kulinda tafiti zake

Thu, 3 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imeitaka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini (NIMR), kulinda tafiti zake kwa ajili ya kuendelea kutoa matokeo bora na yenye tija kwa taifa.

Aidha, imeziagiza taasisi mbalimbali ikiwemo ya Wakala wa Misitu nchini (TFS), kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kama moja ya njia ya kuiwezesha kutekeleza majukumu yake.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge wakati wakifungua maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 1980. Maadhimisho hayo ni ya siku tatu.

Alisema kutokana na umuhimu kwa taifa, NIMR ina kila sababu za kuhakikisha tafiti inazozifanya zinalindwa kwa ajili ya kuziepusha kuibiwa na nchi zingine. Aliongeza kuwa kwa kuruhusu hilo watakuwa wamepunguza ufanisi na sifa ya NIMR.

"Mnapoadhimisha kipindi hiki cha miaka 40, mnapaswa kuhakikisha tafiti zenu zinakuwa salama wakati wote dhidi ya watu wasio na nia njema utendaji wenu, tukiamini kuwa mtaendelea kusimama kama kituo bora cha utafiti wa magonjwa ya binadamu nchini," alisema Kunenge.

Alisema serikali inatambua mchango mkubwa wa taasisi hiyo hususani katika kipindi cha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 ambapo taasisi hiyo ilifanya kazi kubwa na kutengeneza dawa lishe ya NIMRCAF iliyowasaidia wananchi wengi kupambana na ugonjwa huo.

Aliipongeza taasisi hiyo kupitia kituo chake cha NIMR Muhimbili kwa mchango wake mkubwa kwenye tafiti kuhusu Ukimwi na kifua kikuu, ambapo kupitia utafiti wake kimeweza kuleta mabadiliko ya sera na miongozo kwa wagonjwa ndani na nje ya nchi hivyo kuongeza urefu wa maisha ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Yunus Mgaya, alisema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 1980, imetekeleza miradi mingi ya tafiti ikiwemo ya malaria, kifua kikuu na tafiti za magonjwa ya kitropiki zilizotathimini huduma mpya za magonjwa hayo kwa kutumia chanjo.

Sambamba na hilo, alisema pia tafiti hizo NIMR zimefanywa katika maeneo ya magonjwa yasiyoambukizwa na huduma za mama na mtoto, wazee pamoja na vijana.

Alisema katika udhibiti wa tafiti za afya nchini, NIMR imefanikiwa kuanzisha mfumo wa kanuni za kimaadili unaofuata mwongozo na taratibu mahususi za utendaji (SOP)

Chanzo: habarileo.co.tz