Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NIMR: Chanjo corona ni ukoloni mamboleo

Befe53f26d15b23fa8b75fb20d6d9b1f NIMR: Chanjo corona ni ukoloni mamboleo

Mon, 8 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

IMEELEZWA kuwa baadhi ya mataifa yenye nguvu yanabeza teknolojia na mbinu iliyotumiwa na Tanzania chini ya Rais John Magufuli ya kupambana na virusi vya Corona kutokana na kutafuta soko la chanjo zao kwa wananchi wa Tanzania.

Kutokana na ulimwengu kuongozwa na ushindani wa kibishara, kuna makampuni makubwa manne ambayo yanataka kutawala dunia katika usambazaji wa chanjo hiyo.

Makampuni hayo yanatoka katika nchi za Marekani, Uingereza na Ufaransa. Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Dawa (NIMR), Profesa Yunus Mgaya alipokuwa akiwasilisha mada wakati wa kongamano lililokuwa likijadili Umuhimu wa Umajumui wa Afrika katika kutatua changamoto na fursa zinazosababishwa na Covid -19.

Alisema kwa kuwa ugonjwa huo hauna njia moja ya kukabiliana nao ambayo inaweza kutumiwa na mataifa yote, Rais Magufuli alibuni njia ya Kitanzania ambayo kwa asilimia kubwa imeiweka nchi mahali salama.

Profesa Mgaya alisema hakuna haja ya kuwapanikisha (kutia hofu) watu kwa kuwa kiuhalisia ugonjwa huo mpaka sasa umeua watu kwa asilimia 0.03 duniani .

“Hii ina maana kuwa asilimia za watu kuishi katika kipindi cha ugonjwa huo ni asilimia 99.97,” alisema Profesa Mgaya. Alisema Tanzania imechukua hatua sahihi kwa kuwa kwa sasa Tanzania ina wataalamu wa tiba asili zaidi ya 75,000 hivyo njia za kujifukiza, kutumia tangawizi na malimao zimefanyiwa utafiti na mwingine unaendelea ili kuwa na aina mbalimbali za dawa kwa ajili ya kuwatibu Watanzania.

Kwa mujibu wa Profesa Mgaya makampuni makubwa ulimwenguni yanayozalisha chanjo yana lengo la kutawala usambazaji wa chanjo hiyo na kuhakikisha kuwa kila mtu duniani pamoja na Watanzania wanapatiwa chanjo zao ili kujipatia mabilioni ya dola.

Alisema hata chanjo wanazopigia upatu hazina ubora wa kitaalamu kuweza kutumiwa na wanadamu kwa sababu ili chanjo ifikie hatua ya kutumiwa na wanadamu lazima ipitie katika hatua nne kuu.

Hatua ya kwanza baada ya chanjo kutengenezwa inapitia katika hatua ya majaribio ambapo inajaribiwa kwa wanyama kama panya, sokwe na sio binadamu.

Baada ya majaribio kwenda vizuri chanjo inapitia hatua ya pili kwa kupata kibali cha kutangazwa katika majarida ya kisayansi. Profesa Mgaya alisema hatua ya tatu ni ya kujaribisha kwa binadamu wachache kutoka katika mataifa mbalimbali duniani ambapo zoezi hilo litachukua miaka zaidi ya mitatu.

Alisema ikiwa chanjo itafanya vizuri, hatua ya nne ni kujaribiwa kwa watu wengi zoezi linaloweza kuchukua miaka minne na mambo yakiwa mazuri chanjo itasambazwa katika masoko kwa ajili ya biashara katika mataifa mbalimbali.

“Cha ajabu chanjo hii haikuvuka hata hatua ya pili ikapelekwa sokoni hali inayoleta hofu kubwa kwa watumiaji, ndio maana Tanzania tumeamua kuwa na utaratibu wetu wa kushughulikia Corona tupige nyungu sana, tule tangawizi na malimao, tuko salama,” alisisitiza Profesa Mgaya.

Kwa upande wake Mwanamajumui wa Afrika kutoka nchini Afrika Kusini Wakili Sabelo Sibanda alisema Bara la Afrika linatakiwa kutafuta utaratibu wake wa namna ya kushughulika na virusi vya Corona na sio kupangiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Alisema anatamani viongozi wote Afrika wangekuwa na maono kama ya Rais John Magufuli ya kuthamini juhudi za ndani kabla ya kuelekea nje kutafuta msaada kwa kutukuza kazi za nje zenye lengo ovu na maendeleo ya Afrika.

Wakili huyo anayetoka katika Shule ya Kujitambua barani Afrika alisema Tanzania imetoka katika kipindi cha kuelekezwa na kupangiwa cha kufanya na hivi sasa inatoa ujumbe mzuri katika bara la Afrika kuwa inaweza kujipangia cha kufanya na haielekezwi na taifa lolote.

“Afrika ya Kesho inajengwa leo hakuna haja ya mataifa ya Afrika na dunia kuisema Tanzania kwa sababu anachofanya Magufuli ni kuijenga Tanzania ya kesho kwa kuanza na kuweka mipango hiyo leo,” alisema Wakili Sibanda Alisema lengo la mataifa ya Magharibi ni kuona mataifa ya Afrika yanaharibikiwa ndio maana yaliweka mipaka katika ardhi ya Bara hilo ili kutenganisha watu wake na kuzuia jaribio lolote la kuifanya Afrika kuwa nchi moja.

“Ukiangalia Tanzania sasa hivi ni nchi ya kupigiwa mfano Afrika kwa kuthamini rasilimali zake kuanzia madini, utalii, miundombinu na watu wake,” alisema Sibanda.

Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi na Siasa nchini, Roy Sarungi alisema ikiwa Bara la Afrika halitakuwa makini linaweza kupata matatizo kutokana na kulazimishwa na mabeberu kutumia chanjo ya makampuni ya nchi zao.

Alisema tofauti na chanjo za mataifa ya Urusi na China zilizopitia katika hatua zote muhimu kabla ya kuanza kutumiwa na wanadamu, chanjo za mataifa ya Magharibi hazikupitia katika mstari sahihi wa majaribio.

“Tanzania ina bahati ya kuwa na Rais ambaye ni mwanasayansi na mtaalamu wa hesabu, tunatakiwa tukimkosoa Rais Magufuli tujiulize kuwa kwani yeye hiyo sayansi inayolazimishwa na shirika la Afya haijui mpaka achukue utaratibu wake peke yake?,” aliuliza Sarungi

Chanzo: www.habarileo.co.tz