Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NHIF yatupiwa mzigo wa dawa

Mhifpiic Data NHIF yatupiwa mzigo wa dawa

Sun, 7 Aug 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Kutofanyika kwa mabadiliko ya mwongozo wa gharama, kumesababisha vituo hivyo kushindwa kujiendesha na baadhi ya wananchi kunyimwa dawa, huku wengine wakipitia usumbufu mkubwa kupata huduma ya matibabu.

Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa NHIF, Angela Mziray alisema NHIF kwa kushirikiana na wadau wake, umeshakamilisha mapendekezo ya mabadiliko ya bei za huduma na kuwasilisha kwa mamlaka husika.

Gharama ya dawa

Wamiliki wa vituo binafsi katika nyakati tofauti walisema licha ya bei za dawa kupanda, gharama za NHIF zimesalia za mwaka 2016, huku wakitolea mfano wa dawa aina ya paracetamol ambayo wanalipwa Sh20 kwa kidonge wakati wao hununua kati ya Sh35 hadi 250.

Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Afya binafsi Tanzania (Aphta), Dk Egina Makwabe akizungumza jana na gazeti hili, alisema suala la mabadiliko ya gharama limekuwa likijadiliwa kwa miaka mingi bila kufikiwa mwafaka, huku NHIF ukiendelea kutumia gharama za mwaka 2016 licha ya mabadiliko mengi yaliyotokea.

“Kwanza suala la bei ni sugu, bei ambazo watoa huduma wa binafsi na serikalini tunatumia, zilitolewa mara ya mwisho mwaka 2016. Sasa hivi ni mwaka 2022, ni miaka sita na bei haijawahi kubadilika wakati hali imebadilika; kuna bei zimeshuka na nyingine zimepanda kutokana na maisha yalivyo,” alisema.

Dk Makwabe alisema, wagonjwa wanapohudumiwa kwenye vituo vya afya binafsi, NHIF imekuwa ikilipa kulingana na bei ya zamani.

Alitoa mfano wa ongezeko la huduma za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo ‘dialysis’ kwamba awali vituo vilikuwa vichache na sasa kuna vituo zaidi ya 50 vinavyotoa huduma hiyo, hali iliyosababisha gharama kushuka.

“Kuna vitu kama matibabu ya moyo kipindi kile yalikuwa bado duni kwa sasa imebadilika, kuna matibabu mapya ambayo yanagharimu fedha nyingi.

“Mfano dawa ya kutuliza maumivu (paracetamol) mtu mwenye hospitali ananunua Sh35 kwa kidonge hadi Sh250 inategemea na ‘brand’, lakini NHIF itamlipa mtoa huduma Sh20, akitoa ataitoa kwa hasara na mwishowe vituo hivyo vitapata mdororo wa kiuchumi, vitashindwa kulipa kodi na kulipa wafanyakazi,” alisema.

Alisema kuna tofauti kubwa kati ya vituo binafsi na vile vya Serikali ambavyo vinapewa dawa kwa gharama nafuu.

“Hii ndiyo sababu kubwa sisi kama Aphta tunapambana Serikali na wizara, ziweze kutoa bei halisi na zenye uhalisia katika soko,” alisema.

Kauli ya NHIF

Meneja Uhusiano wa NHIF, Angela Mziray akizungumzia mwongozo huo alisema, NHIF kwa kushirikiana na wadau wake imeshakamilisha mapendekezo ya mabadiliko ya bei za huduma na kuwasilisha kwa mamlaka husika.

Alisema NHIF imeshafanya majadiliano na wadau mbalimbali ili kuendelea kupokea maboresho hayo, na baada ya hapo kutoa notisi ya miezi mitatu kabla ya kuanza kwa utekelezaji wake.

Kuhusu mfuko huo kutotambua vituo vingi vya afya vinavyotoa huduma za usafishaji figo kwa wagonjwa, Angela alisema huduma hiyo ipo kwa wanachama kulingana na aina ya uanachama.

“Mojawapo ya majukumu ya mfuko ni kuendelea kusajili vituo vya huduma ili wanachama wake wapate huduma stahiki. Mpaka sasa Mfuko umesajili vituo 46 vya ‘dialysis’ nchini ambavyo vinawahudumia wanufaika wake. Hata sasa Mfuko unaendelea kupokea maombi ya usajili wa vituo na kuyafanyia kazi kwa ajili ya usajili kulingana na miongozo,” alisema.

Akielezea kuhusu ucheleweshwaji wa michango kwa watoa huduma, Angela alisema Mfuko umeboresha ulipaji wa madai kwa watoa huduma kupitia kuimarika kwa mifumo ya Tehama, ambayo inawezesha mifumo ya vituo na NHIF kusomana.

“Mfuko unaendelea kuwasisitiza watoa huduma ambao hawajaunganisha mifumo na NHIF kufanya hivyo ili kumaliza kabisa changamoto hii. Kwa watoa huduma wanaowasilisha madai kwa njia ya mtandao kwa sasa wanalipwa madai ndani ya siku 20,” alisema.

Kero nyingine

Nasoro Nasoro, mkazi wa Mbagala mkoani Dar es Salaam, alitaka mfuko huo kufanyiwa maboresho yenye tija kwa wananchi, kwani wakati mwingine analazimika kutumia fedha zake mfukoni kulipia huduma.

Alisema kwa kutumia bima ya afya, mhusika analazimika kupitia mchakato mrefu wenye usumbufu mwingi, ikiwamo kuzungushwa kabla ya kupatiwa huduma.

“Unaweza kuingia hospitali na bima yako saa 11 alfajiri ukatoka saa tatu usiku; mgonjwa anazungushwa kutwa nzima na hapati matibabu, halafu unaambiwa njoo naye kesho tena. Katika foleni ya kupokea kadi ya bima ya afya watu wanakaa muda mrefu, ukiwa na fedha taslimu nusu saa unatibiwa unaondoka,” alisema.

Changamoto nyingine anayoitaja Nasoro, ni wenye bima kucheleweshewa majibu, kwani kwa kipimo kidogo mgonjwa anaweza kusubiri majibu kwa zaidi ya wiki moja.

Naye Khadija Rashid, mkazi wa Mbezi mkoani Dar es Salaam alisema changamoto kubwa anayopitia anapotumia kadi ya NHIF, ni kuandikiwa dawa ambayo wanapofika kwenye duka la dawa huambiwa bima hailipi au dawa hazipo.

“Pia ukienda hospitali ukiwa unatumia bima si rahisi kutoka mapema ukilinganisha na yule anayelipa papohapo, wakati mwingine kuna idadi maalumu ya wagonjwa wanaotumia bima kutibiwa kwenye hizi hospitali binafsi,” alisema.

Mkazi mwingine wa jijini Dodoma ambaye hakutaja jina lake, alisema: “Kuna siku nilikwenda hospitalini, lakini nilimwona daktari ila dawa nilizoandikiwa, niliambiwa hazipo hivyo nikanunue madukani, sasa hela sina na mimi nilijua bima ndio kila kitu.”

Alisema tatizo la kwenda hospitali na kuambiwa dawa hazipo ni kubwa, huku akiiomba Serikali kuliangalia jambo hilo.

NHIF na ripoti ya CAG

Ripoti ya Mdhibiti na Mdhibiti Mkuu wa Serikali ya Mashirika ya Umma ya mwaka 2020-2021 ilieleza kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mwaka huo ulikataa madai ya Sh3.87 bilioni.

Katika mwaka wa fedha 2020/21, CAG alibaini Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete zilipeleka madai kwenye mfuko yenye thamani ya Sh55.53 bilioni ambapo madai ya Sh 3.89 bilioni yalikataliwa na Mfuko.

Aidha, kwa mwaka 2019/20, madai yaliyokataliwa yalikuwa Sh 3.13 bilioni, hali ambayo inaonyesha madai yanayokataliwa yanaongezeka.

CAG alitaja baadhi ya sababu za kukataliwa ni pamoja na makosa ya ukokotoaji; kukosa maelezo ya huduma zilizodaiwa kutolewa baada ya uhakiki wa madai, hivyo CAG alitoa maoni yake kuwa: “Upo uwezekano wafanyakazi wanaoshiriki kutoa huduma za matibabu kwa wanachama wa mfuko kutofuata taratibu zilizowekwa na zilizokubaliwa kati ya Mfuko na hospitali au vituo vya afya kwa huduma zinazotolewa,” alisema.

“Hali hii inamaanisha hospitali au vituo vya afya hupata hasara kwa huduma za matibabu zinazotolewa kwa wagonjwa kwa kutumia bima ya Taifa ya afya,’’ aliongeza kusema CAG, Charles Kichere.

Maboresho NHIF

Hivi karibuni mfuko huo umekuwa ukifanya baadhi ya maboresho, ambayo hata hivyo yalizua malalamiko, ikiwamo baadhi ya wategemezi wakiwamo wazazi kuanza kuondolewa katika mfumo.

Wakiongeza na Mwananchi, baadhi ya waathirika walisikitishwa na mabadiliko hayo waksema yanaleta usumbufu na kuvuruga matibabu ya wagonjwa wanaotegemea mfuko huo.

Hata hivyo, NHIF ilikiri kuwepo kwa mabadiliko katika baadhi wategemezi, huku Angela akisema wanafanya hivyo ili kurekebisha baadhi ya mianya ya uvujaji wa fedha za mfuko na udanganyifu.

Kadhia nyingine ya NHIF ambayo ilimlazimu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, kuingilia kati na kusitisha Jumatano hii, ni utaratibu uliokuwa ukitaka mwanachama kutumia hospitali moja ndani ya siku 30 na kama anataka kuhama lazima apate rufaa ya hospitali ya awali.

Hatua hiyo iliibuka sintofahamu kwa wanachama katika hospitali mbalimbali hadi Waziri Ummy alipousitisha kwa kudai unaweka zuio la idadi ya mahudhurio kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na utoaji wa kibali kabla ya huduma za vipimo vya MRI, CT SCAN, Colonoscopy, HBA 1C, OGD, USS na ECHO.

“Pamoja na dhamira nzuri ya NHIF ya kutaka kudhibiti udanganyifu unaofanywa na baadhi ya vituo vya kutoa huduma za afya na hivyo kuuweka mfuko katika hatari ya kufilisika, naitaka NHIF kukaa pamoja na wadau ili kujadili na kuja na namna nzuri zaidi ya kuboresha utaratibu huo bila ya kumuathiri mteja pamoja na vituo vyote,” alisema.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz