Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NHIF kuhamasisha bima shule za msingi, sekondari

6164fd7a3cce1342548f8d6a3ce267c2 NHIF kuhamasisha bima shule za msingi, sekondari

Sun, 4 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unatarajia kusajili shule zote za msingi na sekondari ikiwa ni jitihada za kuhakikisha kila mtoto nchini anapata huduma za uhakika za matibabu.

Ofisa Matekelezo wa NHF, Paul Bulolo, aliliambia gazeti hili hivi karibuni jijini hapa kwamba mipango ya usajili iko tayari, ikisubiri ruhusa kutoka mamlaka husika, hasa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

"Ni lazima tusubiri majadiliano na muafaka wa wizara hizi mbili ndio mfuko uanze usajili. Tumejipanga kufikia shule zote ndani ya muda mfupi mara baada tu baada ya kuruhusiwa.

“Tunaamini wazazi wengi wanahitaji huduma kwa watoto wao lakini huenda wengine hawajui watufikieje, hivyo tumeamua kuwafikia kupitia mfumo huu wa kusajili shule. Hata hivyo, kujiunga na huduma zetu ni hiari sio lazima," alisema.

Kwa mujibu wa Bulolo, malipo kwa kila mtoto ni Sh 50, 400 kwa huduma za bima ya afya kipindi cha miezi 12, hata kama (mtoto) atakuwa amevuka miaka 18 ilimradi bado yuko shuleni.

"Hii ni kuwasaidia wazazi kuepuka gharama ambazo wamekuwa wakiingia pindi mtoto asiye na bima ya afya anapougua. Si tu kuepuka gharama bali hata kupata huduma za uhakika kwani bima ni kwa maradhi ya aina zote, madogo na makubwa ambayo huenda baadhi yake mzazi angeshindwa kuyamudu kutokana na kutokua na akiba kwani ugonjwa ni suala la ghafla," alisistiza.

Aliendelea kufafanua kwamba NHIF imekuwa karibu na wazazi katika kutoa huduma za afya kwa watoto kwani hata wale waliopo vyuoni huhudumiwa kwa kiwango kilekile cha Sh 50,400, ilimradi awe anachukua masomo ya shahada ya kwanza na mwenye umri uziodizi miaka 29.

Aliwataka wazazi kujitokeza kwa wingi katika ofisi za mfuko huo hata kwa kipindi ambacho usajili wa shule haujaanza kwa ajili ya huduma za afya kwa watoto wao, wakiwa na uthibitisho wa taarifa za mwanafunzi kutoka shule anayosoma.

Alisema hizo ni jitahada za Mfuko kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za uhakika za afya, muda wowote, katika hospitali yoyote na kwa hiari yake hadi hapo serikali itakapokuwa imetangaza huduma ya bima ya afya kwa wote ambayo itakuwa sasa ni sheria na lazima kwa kila mtanzania kuwa na huduma hiyo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz