Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NHIF kufanya marekebisho ya vifurshi vya matibabu kwa wanachama wake

053eeba35b4d3b2de15e53f6b0a4b747.png NHIF kuongeza wigo kitita cha matibabu

Fri, 3 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema uko katika hatua za mwisho za kufanya mapitio ya kitita cha matibabu ili kuongeza wigo kwa wanachama wa mfuko huo katika kupata huduma zaidi na bora.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga amesema nia ya mfuko wakati huu unapoadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake ni kuboresha huduma na kuongeza ushirikishwaji kwa nia ya kuwapa huduma nzuri na bora kwa wanachama wake na watoa huduma wao.

Konga aliyasema hayo jana mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau ambao ni watoa huduma wa afya kutoka sekta binafsi kutoka mikoa yote Tanzania, ambao mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla aliyewakilishwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Hassan Rugwa.

“Hivi sasa tuko katika hatua za mwisho za uboreshaji wa kitita cha matibabu ili kuwapata wanachama wetu huduma bora na nzuri. Nia yetu ni kuwa na huduma bora zaidi na kuongeza ushirikishwaji,” alisema Konga.

Kwa sasa, kitita cha matibabu cha NHIF kinajumuisha ada ya kujiandikisha na kumwona daktari; huduma za kulazwa; huduma za dawa; vipimo vya maabara na uchunguzi (X-Ray, Echo na EEG, Ultrasound), huduma za kinywa na meno (kung’oa na kuziba meno), huduma za uzazi (kujifungua kawaida na kujifungua kwa upasuaji).

Pia wanatoa huduma za matibabu ya kibingwa na huduma za upasuaji mdogo na mkubwa.

Kwa mujibu wa mtendaji huyo wa NHIF, mfuko pia unalenga kushughulikia suala la ucheleweshaji wa madai ya watoa huduma, kukabiliana na watoa huduma wadanganyifu, na pia kuangalia bei za huduma wanazotoa ambayo nayo mchakato wake umefikia pazuri na umeshirikisha wadau mbalimbali.

Alisema kwa ujumla mfuko umepiga hatua kubwa tangu ulipoanzishwa Julai Mosi, 2001, wakati ulipoanza na vituo ya kutoa huduma 300 vyote vikiwa vya umma, lakini sasa una vituo zaidi ya 8,500 vikiwamo vya umma, sekta binafsi na vya taasisi za dini vinavyowahudumia wanufaika wa mfuko ambao wamefikia milioni 4.8.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF, Juma Muhimbi alisema lengo la mfuko huo ni kutoa huduma zenye ubora, hivyo watahakikisha usimamizi imara ili wananchi wapate huduma bora.

Mwenyekiti wa Umoja wa Watoa Huduma Binafsi za Afya Tanzania, Dk Egina Makabe alisema umoja huo na watoa huduma wake hawapingi suala la serikali kuja na bima ya afya kwa wote, na kwamba itaendelea kushirikiana na serikai katika kutoa huduma bora za afya nchini kwa Watanzania wote.

Aidha, alibainisha kuwa changamoto ya ugonjwa wa Covid-19 imesababisha kuwapo kwa upungufu wa rasilimali watu katika sekta ya afya, pia gharama kubwa za uendeshaji ingawa kwa sasa hali imekuwa na nafuu.

Mgeni rasmi, Mkuu wa mkoa katika hotuba iliyosomwa na Katibu Tawala wa Mkoa aliwataka watoa huduma wasio waamini wanaotoa madai ya udanganyifu kwa NHIF kuacha mara moja, na kwamba katika mkoa wake hatasita kuchukua hatua mara moja kwa wahujumu hao kwani vitendo vyao ni hatari kwa ustawi wa mfuko.

Chanzo: www.habarileo.co.tz