Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NHIF: Tulifanya utafiti wa gharama za vifurushi

86791 Pic+nhif NHIF: Tulifanya utafiti wa gharama za vifurushi

Mon, 2 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wadau nchini Tanzania wakilalamika, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema ulifanya utafiti wa gharama kabla ya kuvitangaza vifurushi vipya vya matibabu.

Kutokana na wananchi wengi kutohudumiwa kwa bima, mfuko huo umesema kwa wiki tatu za Septemba walifanya utafiti unaolenga kuwafikia watu wengi zaidi na wakavuka lengo.

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Desemba 2, 2019 na mkurugenzi mkuu wa mfuko huo, Bernard Konga kwenye kikao na wahariri wa vyombo vya habari nchini Tanzania kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

"Kwa wiki tatu za utafiti, tulilenga kuwafikia kati ya watu 100 hadi 200 lakini tukawapata 700. Kila mmoja alichagua kifurushi akipendacho na tukapata Sh400 milioni," amesema Konga.

Utafiti huo amesema waliufanya katika wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni (zote za Dar es Salaam) kabla hawajaomba kibali cha Serikali kuvitangaza kwa Watanzania wote.

Wiki iliyopita NHIF ilitangaza gharama za vifurushi vipya 66 ambavyo bei zake ni kati ya Sh192,000 kwa mtu mmoja mpaka Sh2.22 milioni kwa familia ya baba, mama na watoto wanne.

Bei hizo, Chama cha ACT Wazalendo kinasema ni kubwa na zitawaumiza wananchi hasa masikini.

Takwimu zilizopo zinaonyesha zaidi ya Watanzania milioni 12 wanaishi chini ya Dola moja ya Marekani kwa siku. Dar es Salaam licha ya kuongoza kwa idadi kubwa ya watu nchini, takriban milioni sita ndio mkoa wenye kiasi kidogo cha umasikini.

Konga amesema NHIF inawahudumia asilimia nane tu ya Watanzania huku asilimia 23 wakiwa chini ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) huku asilimia moja pekee wakihudumiwa na kampuni binafsi za bima.

Chanzo: mwananchi.co.tz