Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NHIF, CHF kuimarishwa Watanzania wote wapate bima

F56d88ee54faf8c480920944bca52c9c NHIF, CHF kuimarishwa Watanzania wote wapate bima

Mon, 12 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuimarisha mfumo wa bima ya afya ikiwa ni pamoja na kuimairisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Amesema Serikali inafanya hivyo ili kufikia lengo la serikali la kuwa na bima ya afya kwa wananchi wote ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Alitoa kauli hiyo alipozungumza na wananchi katika mikutano ya kampeni ya kumuombea kura mgombea urais kupitia CCM John Magufuli, mgombea ubunge jimbo la Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM.

Ilani ya uchaguzi inaelekeza Serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo iendelee kutoa kipaumbele katika sekta ya afya kwa kuwa inagusa maisha ya Watanzania ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora.

Majaliwa alisema awali Serikali ilianzisha NHIF kwa ajili ya watumishi wa umma na baada ya kupata mafanikio ilianzisha CHF, na kwamba, wananchi wanajipangia kiasi cha kuchangia katika maeneo na kuwawezesha kupata huduma za afya bure na familia zao.

"Awali mfuko huu wa CHF uliwezesha wananchi kutibiwa ndani ya wilaya zao tu ambapo kwa sasa umeboreshwa na kuwawezesha kutibiwa ndani ya mikoa yao. Baada ya kupata mafanikio makubwa katika uendeshaji wa mifuko kwa sasa Serikali inaandaa utaratibu wa kutoa huduma za afya kwa Watanzania wote na tayari kazi imeanza kwa muswada kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni."alisema.

Majaliwa alisema changamoto ya upatikanaji huduma za afya katika halmashauri ya wilaya ya Korogwe mkoani Tanga itakuwa historia baada ya Serikali kutoa shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Makuyuni, ambapo tayari ujenzi wa majengo sita umekamilika na jengo moja linamaliziwa.

Pia, Serikali imetoa shilingi milioni 598.6 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Mkumbara na shilingi milioni 200 kimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo kingine cha afya cha Kerenge, na kwamba, ujenzi wa vituo hivyo umekamilika na taratibu za ununuzi wa vifaa tiba unaendelea.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya elimu katika wilaya hiyo, Majaliwa alisema Serikali imetoa shilingi bilioni 3.188 kwa shule za msingi 138 kwa ajili ya ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu.

Alisema, shilingi bilioni 2.50 zimetolewa kwa shule 28 za sekondari kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule.

"Shilingi bilioni 1.410 zimetolewa kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya madarasa, vyoo na ofisi kwa shule 58 ikiwemo ujenzi wa madarasa ya shule za msingi za Mruazi, Gereza, Kwamzindawa, Bombo Majimoto, Mswaha, Lewa na Mkumbara na shilingi bilioni 1.568 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa, vyoo na maabara kwa shule za sekondari za Madago, Mkalamo, Mashindei, Mkomazi, Buiko, Patema, Kwagunda, Mazinde Day, Hale, Mnyuzi na Bungu."alisema Majaliwa.

Chanzo: habarileo.co.tz