Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NGUVU ZA KIUME: Congo ‘Dasti’ yatikisa wanaume, madaktari watoa tahadhari

65399 Shita+Samweli

Thu, 4 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wakati madaktari wakitahadharisha juu ya matumizi holela ya dawa za kuongeza nguvu za kiume maarufu kama Viagra au ‘Congo Dasti’, (Vumbi la Congo) hivi sasa dawa hiyo imeanza kusambazwa kwa kasi.

Licha ya kutotambuliwa na mamlaka za hapa nchini, dawa hiyo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imekuwa maarufu zaidi kwa makundi ya vijana waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda na watu wa umri wa hadi miaka 50.

Dawa hiyo ambayo inaingizwa nchini na wasambazaji wasiojulikana rasmi, imekuwa ikiuzwa kwa Sh15,000 na imekuwa maarufu zaidi mikoa ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro na Jiji la Dar es Saalam.

Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Gaudensia Simwanza, hivi karibuni aliulizwa na Mwananchi juu ya uwepo wa dawa hiyo, alisema TFDA haikuwa na taarifa.

“Ndio kwanza nasikia kutoka kwako kwa hiyo siwezi kuzungumzia jambo ambalo silifahamu labda utuletee hiyo dawa tuione kwanza ndio tunaweza kuisemea,” alisema msemaji huyo wa TFDA.

Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala la Wizara ya Afya, Dk. Edmund Kayombo alipoulizwa jana alisema vumbi hilo anasikia tu kupitia mitandao ya kijamii ila haijasajiliwa nchini.

Pia Soma

“Kwa kweli hiyo dawa mimi siifahamu. Niliwahi kusikiasikia Vumbi la Congo, Vumbi la Congo lakini sikuwahi kujua ipo. Sisi dawa pekee ya kuongeza nguvu za kiume tuliyoisajili ni Ujana,” alisema.

Watumiaji wadai ni moto mara moja

Mmoja wa watumiaji wa dawa hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema maelekezo ni kwamba mtumiaji hulipaka vumbi hilo katika kichwa cha uume na ndani ya dakika 30 inafanya kazi.

“Usije ukanitaja huko kwenye magazeti yako ila mimi bila hiyo naona kama sifurahii tendo lenyewe naona nimekuwa kama mgonjwa vile. Ukishaitumia tu ‘jamaa’ husimama kwa muda mrefu,” alidai.

Mfanyabiashara wa mitumba soko la kimataifa la King George Memorial la mjini Moshi, alisema amekuwa akiinunua dawa hiyo ikiwa katika kichupa mithili ya bomba la sindano kwa Sh15,000.

Dereva wa bodaboda anayeegesha pikipiki yake stendi kuu ya mabasi, alidai dawa hiyo ina uzuri wake na ubaya wake na kwamba ubaya ni pale utakapoipaka halafu mwenza wako akukatalie.

‘Unajua hilo vumbi linapoletwa linakuwa limewekwa kwenye kichupa kama bomba la sindano hivi. Kwa hiyo kwanza unapaka mate au lotion (mafuta) kwenye ‘kichwa” ni nusu saa tu,” alidai.

Mfanyabiashara huyo alidai ameamua kuondokana na matumizi ya Viagra za kumeza kwa kuwa wakati mwingine zinamletea athari ikiwamo kuumwa na kichwa, kusikia kichefuchefu au kutapika.

Madaktari watahadharisha watumiaji

Dk Shita Samwel alisema kitabibu kutumia dawa yoyote bila kuthibitishwa TFDA ni hatari kwani bila kujua usalama wake ni kujiweka katika hatari ya kifo au madhara makubwa ikiwamo yale ya kudumu.

“Kwa taarifa kadhaa za mitandaoni wanaoitangaza dawa hii ni kuwa inaongeza kwa kusisimua mishipa ya damu na ya fahamu na kuufanya uume kusimama kwa muda mrefu,” alisema Dk Shita.

“Dawa kama hii haijatafitiwa na wanasayansi wa tiba na madawa hivyo ni vigumu kujua dose (kiwango) kwa mtumiaji ambacho kitakuwa ni salama. Hii ni hatari sana kwa mtumiaji,” alisisitiza.

“Watu wanatumia dawa hiyo kiholela kwa mujibu ya maelekezo ya wauzaji ambao si watalaama wa dawa bali wanatumia uzoefu wa kihistoria wa dawa hiyo toka nchini Congo. Hii si sawa.”

“Jambo kama hili linaweza kuchangia watumiaji kupata madhara kadhaa ya kiafya ikiwamo tatizo lijulikanalo kama Priapism yaani uume kusimama zaidi ya saa 4 kwa muda mrefu bila kusinyaa”.

Dk Shita alisema tatizo hilo huwapata watumiaji wa dawa za kuongeza nguvu huambatana na maumivu makali na hatua za kitiba zisipochukuliwa mtu anaweza kupoteza nguvu za kiume kabisa.

“Zipo pia taarifa nyingine za watumiaji wengine ambao hata hawana tatizo bali huzitumia dawa hizo kutokana na ushawishi wa makundi ya vijiweni na matangazo nao hujikuta wakizitumia,” alisema.

“Hapa matokeo yake ni kuathirika kisaikolojia yaani hata kama alikuwa hana tatizo la nguvu la kiume akili yake hujijengea hisia kuwa bila dawa hizo hawezi kushiriki tendo la ndoa,” alifafanua zaidi.

Daktari katika hospitali ya TPC iliyoko Moshi Vijijini, Dk Timizael Sumuni alisema matumizi ya dawa hiyo ni hatari kwa vile haijulikani ina mkusanyiko (ingredients) kiasi gani na ina nguvu kiasi gani.

Dk Sumuni alisema ni vyema wanaohisi wana matatizo ya nguvu za kiume wakamuona daktari kwanza kwani pengine wanaweza kuwa na tatizo katika mifumo ya homoni au mishipa ya fahamu.

Kwa mujibu wa Dk Sumuni, wengine wanaweza kupoteza nguvu za kiume kutokana na msongo wa mawazo au kuathirika kisaikolojia hivyo tiba yake si kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume.

Jinsi inavyotangazwa mitandaoni

Katika ukurasa wa Facebook, msambazaji mmoja ameweka tangazo akisema vumbi hilo la Congo linapatikana kwa Sh10,000 na kwamba msambazaji huyo anapatikana Ilala Bungoni jijini Dar.

“Inapatikana pia mikoa ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Kahama, Nzega, Shinyanga, Mbeya, Geita, Chato, Sengerema, Katoro na Buselesele,” ameeleza msambazaji huyo na kuongeza, “Kwa mikoa mingine pia msiwaze sana tunatuma popote Tanzania na utalipa utakapopokea dawa hii, nitafute kwa simu namba (imehifadhiwa) piga simu muda wowote masaa 24”

Katika mtandao huo, msambazaji huyo anadai baada ya kuitumia, mtumiaji atadumu katika tendo la ndoa kati ya dakika 35 na saa moja na kwamba ni dawa salama kulinganisha na za viwandani.

Chanzo: mwananchi.co.tz