Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwongozo wa serikali na jinsi ya kuhudumia waliothirika na ukatili wa kijinsia

835b2965d6fd9705a77f14f47f583b69 WAZIRI wa Afya, Dk Dorothy Gwajima akizundua mwongozo wa serikali

Fri, 1 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima, amezindua mwongozo wa sera ya nyongeza ya ushirikiano wa majukumu baina ya kada za afya kuhusu ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na ujazaji wa fomu namba 3(PF3).

Mwongozo huo unatoa mfumo wa huduma bora na toshelezi zinazojumuisha matibabu, rufaa, huduma za msaada wa kisaikolojia na kijamii zinazohusiana na ulinzi wa kisheria kwa watu wanaopatwa na ukatili wa kijinsia.

Akizungumza baada ya kuzindua, Dk Gwajima, alisema sera hiyo ya nyongeza ni nyenzo muhimu kwa wasimamizi na watoa huduma za afya huku akielekeza wizara kuhakikisha unapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma nchini.

Hata hivyo, Dk Gwajima alisema kesi nyingi za ukatili wa kijinsia na udhalilishaji zimekuwa zikishindwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi.

Alibainisha ujio wa mwongozo huo wa sera ya nyongeza ya ushirikiano wa majukumu baina ya kada za afya kuhusu ukatili wa kijinsia, ukatili dhidi ya watoto na ujazaji wa PF3 utawajengea uwezo wa kuwahudumia waathirika ikiwemo kuchukua au kutoa ushahidi pale unapohitajika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania Interfaith Partnership (TIP), Saida Mukhi, alisema mchakato umechukua miaka miwili, hadi kukamilika kwa sera ya nyongeza ya ushirikiano wa majukumu dhidi ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto baina ya kada za afya.

"Tunaishukuru Wizara ya Afya kwa kulipa umuhimu jukumu hili na kufanya kazi bega kwa bega na TIP kufanikisha," alisema.

Mwenyekiti TIP na Katibu Mkuu Ofisi ya Mufti Zanzibar, Shehe Khalid Mfaume, alisema takwimu za Shirika la Afya duniani zinakadiria kuwa takribani wasichana milioni 150 na wavulana milioni 73 chini ya umri wa miaka 18 wamekwisha fanyiwa vitendo mbalimbali vya ukatili na udhalilishaji.

Chanzo: www.habarileo.co.tz