Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwongozo wa malezi kwa watoto wadogo waandaliwa

Sat, 22 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jumla ya vituo 1,325 vya kuhudumia watoto wadogo vimesajiliwa nchini huku vingi vikiwa vinaendeshwa bila utaratibu kutokana na kukosekana kwa mwongozo.

Hilo linachangia watoto kukosa malezi sahihi kutoka kwa wataalam ambao wamebobea kutoa huduma, malezi na ulinzi kwa watoto.

Kufutia hali hiyo, Serikali kwa kushirikiana na shirika la maendeleo la Brac Tanzania imeandaa mwongozo wa malezi kwa watoto.

Ofisa ustawi wa jamii mwandamizi kutoka wizara ya afya, Elekta Kilusungu akizungumza  leo Septemba 20, 2018 amesema kutokuwepo kwa mwongozo kunawafanya waviendeshe vituo hivyo kiholela.

Akizungumza wakati wa mkutano wa kukusanya maoni ya kuboresha rasimu ya mwongozo wa malezi Kilusungu amesema vituo hivyo ni muhimu ila vinapaswa kufanya kazi kwa utaratibu unaofaa.

"Tuna vituo 1,325 na vinahudumia watoto 4,979. Hii ni idadi kubwa tunapaswa kuhakikisha vinafanya kazi iliyokusudiwa na hilo litawezekana kukiwa na mwongozo,"

“Vituo hivi vya kulelea watoto mchana ni taasisi muhimu katika kutoa huduma za uchangamshi wa awali kiakili, mwili, hisia na maadili," amesema Kilusungu.

Kwa upande wake, meneja wa programu ya Elimu wa Shirika la Brac Tanzania, Susan Bipa amesema mwongozo huo umekuja kutatua changamoto zinazozunguka uwepo wa vituo hivyo.

Amesema kwa sasa wazazi wamekuwa wakiwapeleka watoto kwenye vituo hivyo na kuacha majukumu yote kwa walezi.

"Mwongozo unataka wazazi washiriki kikamilifu kwenye malezi si kuwaachia tu jukumu hilo walezi wa day care," amesema Bipa.

Chanzo: mwananchi.co.tz