Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwelekeo mpya kuhusu bima ya afya kwa wote

Ummy Mwalimu Uviko.jpeg Mwelekeo mpya kuhusu bima ya afya kwa wote

Sun, 12 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati wadau wakipendekeza vyanzo vya fedha zitakazotumika kugharamia huduma za afya kupitia mfumo wa Bima ya Afya kwa wote, takribani Watanzania milioni 16.2 watapata changamoto za kuchangia huduma hizo.

Kwa mujibu wa Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi (HBS) wa mwaka 2017/18 ulionyesha zaidi ya robo wananchi wa Tanzania Bara (asilimia 26.4) hawakuweza kumudu mahitaji yao ya msingi.

Kwa kiwango hicho, kwa idadi ya watu waliokuwepo nchini kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 (milioni 61.7) Watanzania milion 16.2 hawakuweza kumudu mahitaji yao ya msingi.

Idadi hiyo inajumuisha Watanzania wasioweza kumudu mahitaji yao ya msingi wenye wastani wa pato la Sh49,320 kwa mwaka, ikiwa Serikali itatafuta vyanzo vya fedha itatumia Sh977.98 bilioni ambayo ni sawa na asiliM 2.4 ya bajeti kuu ya mwaka wa fedha 2022/23.

Kwa mujibu wa mapendekezo mapya ambayo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliliambia Mwananchi Desemba 2022, kulikuwa na maboresho ya muswada huo ambapo bima mbili ziliwekwa.

Bima hizo moja itakayomwezesha mtu kutibiwa katika hospitali za Serikali na binafsi popote alipo, pamoja na bima ya kitita cha huduma za msingi ambayo itamwezesha mtu kutibiwa katika zahanati, kituo cha afya na hospitali ya wilaya popote nchini kwa gharama ya kati ya Sh60,000.

Hii ina maana Mtanzania maskini anahitaji kutenga takribani asilimia 10 ya kipato chake kwa huduma za afya kwa mwaka, kwani wastani wa pato lao kwa mwaka ni Sh591,840.

Mchanganuo huo umekuja siku moja tangu muswada huo wa bima ya afya kukwama tena kuwasilishwa bungeni, chanzo kikielezwa kukosekana kwa taarifa sahihi za vyanzo vya fedha vitakavyowezesha utaratibu huo kuwa endelevu.

Muswada huo ambao ulitarajiwa kusomwa kwa mara ya pili juzi na kujadiliwa kwa siku mbili kabla ya kupitishwa na Rais kuwa sheria kamili, uliondolewa huku Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akisema majadiliano bado yanaendelea kwa lengo la kuuboresha.

Hata hivyo, taarifa zilizolifikia Mwananchi, kutoka katika kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika Jumatano usiku kilitawaliwa na mvutano mkubwa na kwenye Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii iliyopitia muswada huo.

Taarifa hizo zinaeleza wabunge walikuwa wakali baada ya Serikali kuonekana haina takwimu za kiasi cha fedha kitakachotumika kuutekeleza.

Wasio na uwezo kabisa

Hata hivyo, ripoti hiyo ilionyesha Mtanzania mmoja kati ya wanane ni maskini sana sawa na Watanzania milioni 4.1 kwa mwaka 2017/18.

Kwa makadirio ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Watanzania waliopo kwenye kundi hilo ni milioni 4.8.

Kwa makadirio ya kipato cha kundi hili watahitaji kutenga asilima 15 ya kipato chao cha Sh404,976 wanachopata kwa mwaka na iwapo Serikali itagharamia itatumia Sh288.47 bilioni kwa mwaka.

Vyanzo vya fedha

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Deusdedit Ndilanha alitaja maeneo matano ambayo Serikali inatakiwa kuchukua fedha ambayo ni ya uhakika kugharamia huduma za afya.

“Serikali iangalie kuna vyanzo vingi vyya fedha, iangalie kuweka fedha kwenye mfuko wa afya kwa kuchukua asilimia ya mapato kutoka kwenye maliasili tulizonazo kama vivutio vya utalii au migodini,” alisema.

Alitaja vyanzo vingine kuwa ni kuweka kodi kwenye vyakula hatarishi kwa afya kama pipi, biskuti na vyakula vya kwenye makopo pamoja na eneo la vinywaji hatarishi ikiwemo soda na pombe.

“Ichukuliwe hata Sh50 mwisho wa siku tukajikuta tuna fedha nyingi, kuna fedha zinaenda Ewura au REA ambayo tunaona imefanikiwa kwa asilimia 95 wangetumiia mfumo huohuo na haitaogeza mzigo kwa mwananchi,” alisema.

Pia Dk Ndilanha alisema Serikali inatakiwa kuchukua asilimia kwenye kampuni za bahati nasibu na asilimia kadhaa kutoka bima za vyombo vya moto.

Mkufunzi wa chuo cha Afrika cha bima na hifadhi ya jamii (ACISP), Anselim Anselim alisema wastani wa matibabu ya Watanzania wote kwa mwaka ni Sh7 trilioni na wastani wa matumizi ya pombe kwa nchi ni Sh12 trilioni, hivyo inaonyesha nchi inatumia zaidi kwenye pombe kuliko matibabu.

“Lakini bado tunaona matibabu gharama, tunaweza kuangalia sehemu gani wananchi wanatumia zaidi, mfano jijini Dar es Salaam kuna watu wanatumia Sh200,000 mpaka Sh300,000 kwa usiku mmoja katika pombe, kwanini tusichukue fedha huko kwenye matumizi yasiyo ya muhimu zisaidie afya za watu. Pia tukaangalia kwenye sigara, soda na vingine,” alisema Anselim.

Naye Naibu Msemaji wa sekta ya afya, Ruqayya Nassir kutoka chama cha ACT- Wazalendo, alisema waliishauri Serikali itenge kila mwaka katika bajeti yake asilimia 2.5 ya pato la Taifa kama fedha za kuchangia mfumo huo wa afya kwa thamani ya sasa ambayo ni sawa na Sh3.5 trilioni.

“Serikali haitakuwa tena na jukumu la kuendesha vituo vya kutoa huduma za afya, kwani kwa mfumo huu vituo vitajiendesha vyenyewe na kwa ufanisi mkubwa,” alisema.

Pia chama hicho kilipendekeza kila mwananchi mwenye ajira rasmi na kukatwa michango ya hifadhi ya jamii apate fao la matibabu ambapo mfuko wa NSSF au PSSSF ambao mwajiriwa mchango wake 1/5 upelekwe kwa skimu ya bima ya afya.

“Kila mwananchi aliyejiajiri kwenye sekta yeyote ikiwemo kilimo au shughuli nyingine yeyote na ni mwanachama wa hiari katika mfuko huo anayechangia kiwango cha chini cha mchango wa mwezi Sh30,000 achangiwe na Serikali theluthi ya mchango kila mwezi,” alishauri Nassir.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live