Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwathirika mimba za utotoni alaumu wazazi

D7ee1c9d975bccbe9b9d537073da25a1 Mwathirika mimba za utotoni alaumu wazazi

Sun, 19 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WASICHANA waliopata ujauzito katika umri mdogo hupitia vipindi vigumu wakati wa kulea mimba hadi kujifungua baada ya waliowapa ujauzito kukimbia na kuwaacha bila msaada wowote, imefahamika.

Mmoja wa waathirika wa mimba wa utotoni, mwenye umri wa miaka 19 (jina tunalo) Mkazi wa Kijiji cha Chalinze Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma alisema maisha yalibadilika baada ya kupata ujauzito.

Hata hivyo alisema kupata mimba kwake kulitokana na hali ngumu ya maisha nyumbani kwao.

“Sio kila anayepata mimba ni mhuni au alipata kwa kujitakia kutokana na tamaa zake, wazazi wangekuwa wanatimiza wajibu wao kwa familia, hizi mimba nyingi zisingekuwepo, unalala na njaa na kesho unatakiwa uamke kwenda shuleni na ni mbali na ushinde na njaa hata ukisoma unakuwa huelewi kitu,"alisema.

Alisema wasichana wanaopata ujauzito katika umri mdogo wengi wao huishia kutelekezwa na kuonekana kama mzigo kwa familia.

"Nilikata tamaa baada ya kuharibu msingi wa maisha kutokana na kupata mimba nikiwa shuleni jambo hili liliniumiza sana maana familia yetu ni maskini, nilitamani kusoma ili niwe msaada hata kwa wadogo, zangu,”alisema.

Alisema hakuweza kumaliza elimu ya msingi na hivyo kujikuta akiwa mama katika umri mdogo.

"Nilikuwa nikisoma Shule ya Msingi Chibulunje, nilifukuzwa shule kutokana na ujauzito wakati huo nilikuwa darasa sita, siku hiyo siwezi kuisahau,"alisema.

Akizungumza katika mahojiano alisema alianza kujigundua yeye mwenyewe baada ya kukosa siku zake kwa miezi mitatu.

"Baba wa mtoto hayupo, alishakimbia baada ya mimi kugundulika kuwa ni mjamzito na nilijikuta naingia katika mapenzi kutokana na maisha magumu. Kwani alilazimika kununulia vifaa vya shule na wakati mwingine chakula ili nisishinde njaa,"alisema.

Hata hivyo alisema baada ya mtoto wake kufikisha mwaka moja alipata kijana mwingine ambaye alikuwa akimsaidia fedha ndogo ndogo za matumizi lakini baadaye akajikuta wakiwa wapenzi na kupata ujauzito mwingine.

"Hapa nina watoto wawili na wote bado wadogo, hata aliyeniahidi kunioa naye kanikimbia,"alisema.

Alisema hali yake ya sasa ni mbaya zaidi kwani hawezi kujitunza mwenyewe wala watoto wake na kwamba mama yake ndiye anawatunza yeye na wanawe.

Mratibu wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Women Wake UP (WOWAP) linalotekeleza mradi wa kutokomeza mimba na ndoa za utotoni katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Nasra Suleiman alisema umaskini umeonekana kuwa chanzo kikubwa cha wasichana kupata mimba wakiwa na umri mdogo.

"Wazazi wanashindwa kuwatimizia watoto wao mahitaji muhimu ya maisha ikiwemo chakula,”alisema.

Pia alisema tatizo la mimba kwa wanafunzi linatokana na changamoto ya mazingira na uchumi wa kaya kwa ujumla.

Alisema wazazi wengi hawana muda wa kufuatilia watoto wao wako wapi na katika maeneo mengine watoto wanaambiwa wajiongeze ili waweze kupata mahitaji.

Mratibu huyo alisema jamii ina wajibu wa kuhakikisha inakuwa na dhamira ya kulinda watoto wa kike ili waweze kufikia ndoto zao.

"Sababu kubwa za mimba za utotoni ni watoto wengi wa kike kukosa elimu inayohusiana na madhara ya mimba za utotoni. Pia baadhi yao kutoelewa mabadiliko wakati wa kupevuka na kushindwa kuhimili mihemko,"alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz