Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanza kufanya tathimini ya afya, corona, UKIMWI

D26f3bb79782b896a13aaba270b5a981.jpeg Mwanza kufanya tathimini ya afya, corona, UKIMWI

Wed, 28 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali mkoani Mwanza zinazowajumuisha wakuu wa wilaya zote saba, wakurugenzi wa halmashauri, ofisi ya mganga mkuu wa mkoa, katibu tawala wakiongozwa na mkuu wa mkoa Mhandisi Robert Gabriel leo wamekutana na kufanya tathmini ya mkataba wa lishe, chanjo mpya ya Covid-19, UKIMWI na afya ya mama na mtoto.

Kikao hicho kimelenga kujadiliana namna utekelezaji wa masuala hayo yanavyofanikiwa ikiwa ni pamoja na kutafuta mbinu mpya zitakazo saidia kuepuka vikwazo katika utekelezaji wake.

Akifungua kikao hicho mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel amesema chanjo mpya ya virusi vya corona ipo nchini na kuwataka viongozi katika ngazi za chini za serikali kutumia muda wao kutoa elimu kwa ufasaha ya namna chanjo hiyo itakavyotolewa pamoja na kuwafahamisha umuhimu wake ili kuondoa sintofahamu iliyopo juu ya ubora wa chanjo hiyo.

“Mheshimiwa Rais ameunda tume ya wataalamu wa afya wabobezi na wametuandalia utaratibu nini tufanye kama mkoa na nini tufanye kama nchi, watatuambia chanjo zilizopo na tutazizindua sisi tuliopo hapa” Alisema mkuu wa mkoa.

Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mh.Amina Makilagi amezungumza na kusema wananchi wawe tayari kuipokea chanjo hiyo kwakuwa inaumuhimu mkubwa sana katika kunyanyua kinga mwili ya binadamu na kwakufanya hivyo itawasaidia kujikinga na maradhi ya Corona huku akiongeza kuwa mataifa yanayotengeneza chanjo hiyo hayana nia ovu kama watu wanavyodhani.

“Rais wetu ana nia njema na watanzania na haya mataifa yanayotengeneza chanjo tunashirikiana nayo katika chanjo mbalimbali kama chanjo ya UKIMWI, chanjo za watoto na wanawake wajawazito hivyo wangekuwa na dhamira mbaya tungesha ondoka wote”. Alisema Amina Makilagi.

Mkurugenzi mtendaji wilaya ya magu Lutengano Mwalwiba amesema wananchi wanatakiwa kuacha wataalam wafanye kazi yao ili kuondoa hofu kwa watu na wale walioko tayari basi waweze kupata chanjo hiyo na kusisitiza watu kuweka siasa katika chanjo hiyo na kuvuruga utaratibu.

“Timu ya mkoa imeshajipanga na baadaye wataainisha vituo vya chanjo sasa jukumu letu ni kupeleka taarifa sahihi kwa wananchi ili wapate uelewa na utayari wa kupata chanjo hiyo. Serikali imefanya mengi sana kwaajili ya kuweza kuokoa watu wake”. Alisema.

Viongozi hao wa mkoa wataendelea na kikao hicho tena hapo kesho wakijadili namna ya kuokoa maisha ya mama na mtoto wakati wa kujifungua pamoja na kusisitiza elimu ya Ukimwi kwa vijana ikiwa ni mkakati mmojawapo wa kupambana na gonjwa hilo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz