Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muuguzi aliyempiga mjamzito aondolewa orodha ya wauguzi

B2e745a0b5235bd5dc4814b3db35c2de Muuguzi aliyempiga mjamzito aondolewa orodha ya wauguzi

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

BARAZA la Uuguzi na Ukunga Tanzania limemuondoa kwenye orodha ya wauguzi na wakunga baada ya kumkuta na hatia muuguzi wa kituo cha afya Mazwi, Valentine Kinyanga kwa kumpiga vibao mama aliyefi ka kujifungua kituoni hapo Januari 5, mwaka huu.

Hatua hiyo imechukuliwa chini ya kifungu 28(3) (a) cha sheria ya uuguzi na ukunga Tanzania ya mwaka 2010 na kutakiwa kurejesha vyeti na leseni kwa muuguzi mkuu wa mkoa wa Rukwa ambaye atawasilisha kwa Baraza.

Akisoma hukumu hiyo juzi mbele ya wakili wa Serikali, Fortunatus Mwandu, Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Abner Mathube, alisema baraza limemtia hatiani mlalalamikiwa chini ya kifungu 26(a)(c) ya sheria ya uuguzi na ukunga kwa kosa la kwanza na la pili.

Mathube alisema kuwa baraza lilichambua maelezo ya mlalamikiwa, mlalamikaji pamoja na mashahidi kuhusu kosa la kwanza la kumpiga mgonjwa kinyume na kifungu 25(3)(c)cha sheria ya uuguzi na ukunga Tanzania.

Katika kosa la kwanza lililotolewa ushahidi ulithibitisha mlalamikiwa alimpiga mlalamikaji na mtuhumiwa alikiri kufanya hivyo.

Aidha, kosa la pili lilikuwa ni kushindwa kusimamia maadili na weledi wa kitaaluma kinyume na kifungu 25(3)(k) lilithibitika kwa mtuhumiwa kushindwa kufuata utaratibu wa utoaji wa huduma za uuguzi na ukunga kwa mlalamikaji.

Pia kushindwa kuchukua na kuhifadhi taarifa za vipimo vya mgonjwa, kushindwa kufuatilia mwenendo wa uchungu wa mgonjwa wakati wa kumpokea katika kituo cha kutolea huduma na kuruhusu mtu ambaye sio mtaaluma kumpima mlalamikaji (mgonjwa)

Akizungumzia adhabu aliyopewa ya kuondolewa kwenye orodha ya wauguzi na wakunga, mwenyekiti huyo wa baraza alisema haki ya rufaa imeelezwa chini ya kifungu 31(1) cha sheria ya uuguzi na ukunga Tanzania ambapo anaweza kukata rufaa kwa waziri mwenye dhamana ndani ya miezi mitatu tangu tarehe ya hukumu.

Januari 5, mwaka huu saa 4 usiku, ilidaiwa Kinyanga alimpiga vibao Zulfa Said ambaye alifika kituo cha afya Mazwi kujifungua. Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania lilifuatilia tuhuma hizo na hatimaye kumkuta na hatia.

Chanzo: habarileo.co.tz