Kazi ya uuguzi ni wito. Ndivyo wengi wanavyopenda kusema. Pamoja na ukweli kwamba kazi hiyo ni wito lakini ni ngumu na yenye changamoto mbalimbali na hivyo kuifanya kwa muda mrefu si jambo dogo. Kati ya waliofanya kazi hiyo kwa muda mrefu ni Haulat Amir Daudi aliyeifanya kuanzia mwaka 1984 hadi sasa. Katika utendaji wake huo wa miaka 35 amefanya kazi ndani ya majukumu yake na nje kulingana na mazingira yanayojitokeza kwa wakati husika. Humo humo kuna kuzalisha, kutoa huduma za dharura na hata kujitoa mhanga kuhakikisha hali ya mgonjwa inakuwa sawa kabla daktari hajawasili yamekuwa ni maisha yake tangu enzi za usichana wake.
Haulat aliyeanza kazi Agosti mwaka 1984, anasema aliipenda kazi hiyo tangu akiwa mdogo na malengo yake ilikuwa ni kuja kuwa muuguzi ili ahudumie jamii inayomzunguka.
Kipindi chote cha kazi yake, Haulat amekuwa akihudumu zaidi katika wodi za upasuaji, alianza kazi katika Hospitali ya Wilaya Monduli mkoani Arusha, kukiwa na idadi ndogo ya wauguzi na watoa huduma za afya.
“Nilianza kazi katika wodi za kawaida, wauguzi hawakuwa wengi kwangu sikuona ni changamoto kwa kuwa niliangalia zaidi nini yalikuwa matamanio yangu katika maisha, kuhudumia wagonjwa wengi kwa wakati mmoja ilinipa ari zaidi ya kujituma,” anasema.
Anasema akiwa Monduli alifanya kazi katika kitengo cha upasuaji na alikuwa muuguzi katika wodi hizo. “Nilikuwa nafanya kazi katika chumba cha upasuaji, nikiwa muuguzi peke yangu hata hivyo kulikuwa na mtoa huduma mmoja. Wakati mwingine nililazimika kufanya kazi katika wodi za kawaida na huko kulikuwa na kiongozi mmoja pamoja na ‘attendant’ wawili,” anasema.
Anasema kwamba mazingira hayo ya kazi japokuwa yalikuwa ni magumu yasingemwezesha kuichukia kazi yake.
“Nilijitoa kwa kazi hiyo, kwa kuwa niliishi katika nyumba ya wafanyakazi hospitalini, hapo sikuona shida hata alipotokea mgonjwa wa dharura nikaamshwa usiku kwa ajili ya kumhudumia, nilienda chumba cha upasuaji nilitoa huduma na nilipohakikisha mgonjwa yupo sawa nilirudi nyumbani na kulala,” anasimulia Haulat kuhusu maisha yake ya uuguzi.
Baada ya kufanya kazi kwa miaka saba, maisha ya Haulat yalipitia hatua nyingine, alipata mchumba na kuolewa mwaka 1991.
Huo ulikuwa mwanzo mpya wa maisha yake na kwa kuwa mumewe aliishi na kufanya kazi jijini Dar es Salaam, Haulat ilibidi amfuate mumewe, alipata uhamisho kutoka Monduli na kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kuanza upya utoaji huduma katika hospitali hiyo ya rufaa.
“Nilipewa jukumu la kutoa huduma ya uuguzi katika wodi namba 2 lakini zilikuwa ni za upasuaji, huku majukumu yaliongezeka na safari hii nilianza kutoa pia huduma kwa wagonjwa wa ajali, hii ni kwa kuwa huduma zote za upasuaji zilikuwa zikifanyika Muhimbili,” anasema.
Japokuwa alitoa huduma kwa wagonjwa wote, aliegemea zaidi wagonjwa wa ajali kwani wakati huo kitengo cha mifupa kilikuwepo lakini hakikujitenga kama ilivyo sasa mpaka kilipoanzishwa rasmi.
Haulat ambaye amekuwa muuguzi kwa takribani miaka 23 katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi) tangu ilipoanzishwa mwaka 1996, kuhudumia wagonjwa wa ajali imekuwa sehemu ya maisha yake.
Kwa miaka hiyo aliyotoa huduma rasmi katika kitengo hicho, Haulat anasema amefanya mengi akiwa katika kutekeleza majukumu yake lakini yapo mengi pia aliyafanya nje ya majukumu yake lakini hachukulii kama changamoto kwani jukumu lake ni kuokoa uhai.
“Nakumbuka miaka minne nyuma nilishazoea kutoa huduma kwa wagonjwa wakiwa wamelala chini, licha ya kwamba iliniumiza sana lakini binafsi nilikuwa nikipata matatizo ya mgongo, miguu kuuma na kuvimba yaani nilikuwa nikirudi nyumbani naweka miguu juu ya stuli watoto wananikanda na wakati mwingine hata kichwa.”
Haulat anasema licha ya yeye kutoa huduma kwa shida kwa kuchuchumaa au kuinama, ilimtesa sana rohoni mwake kwa kuwa wagonjwa wengi wa ajali hawakuwa na ndugu hivyo kulala chini kuliwaongezea maumivu na kuwapotezea matumaini.
Anasema ujenzi wa jengo jipya la Moi umewawezesha wauguzi kufanya kazi kwa wepesi zaidi na kusaidia wagonjwa vizuri ikilinganishwa na awali.
“Zamani kulikuwa na tatizo mgonjwa anataka kupewa dripu lakini amelala chini inakuwa ni vigumu kumpa huduma japokuwa atazipata zote lakini kwa ugumu,” anasema.
Akizungumzia nyakati ngumu za kufanya kazi ambazo Haulat amewahi kuzipitia, anasema ni kuhusu malipo ya wagonjwa.
“Wagonjwa tumekuwa tukitofautiana nao nyakati zingine, anapokea huduma lakini kwa kuwa hana bima unapomwambia inatakiwa uchangie huduma wengine wanaona kama ile fedha unaihitaji wewe, baada ya kuja mfumo wa kulipia kielektroniki imekuwa rahisi kuhudumia, zamani jukumu la kukusanya malipo lilikuwa letu.
Licha ya majukumu aliyonayo, Haulat anasema kubwa kuangalia ilikuwa ni familia yake.
Mama huyo wa watoto watatu Asna, Yuneth na Millsent anasema haikuwa kazi rahisi katika ulezi wa watoto wake ijapokuwa wamepishana umri kwa kiwango kikubwa.
“Mtoto wangu wa pili ndiye aliyenisumbua zaidi katika malezi, akiwa mdogo alikuwa anaumwa mara kwa mara hilo lilinifanya nishindwe kutekeleza majukumu yangu ipasavyo, nakumbuka nikiwa kazini siku moja nilipigiwa simu mtoto amezidiwa, kila nikiomba ruhusa sikuweza kuruhusiwa hilo liliniuma sana ila nilijipa moyo kuwa nikitoa huduma sahihi kwa wagonjwa nitamkuta mwanangu na Mungu atamsaidia,” anasema.
Haulat anasema wakati huo watoa huduma walikuwa wachache, kwa upande mmoja alimuelewa bosi wake lakini kuna nyakati pia alishindwa kuelewa.
Miaka 35 ya kutoa huduma, Haulat anasema imemweka katika nafasi nzuri na aliweza kutoa huduma hiyo hata kwa mama yake aliyeugua kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.
“Baba yangu alikuwa muuguzi ndiyo maana nilipenda kazi hii. Mimi na mdogo wangu ni wauguzi, kazi hii imeweza pia kusaidia familia. Mama yangu alilala kitandani miaka mitano, tulikuwa tukipeana zamu kumuuguza imesaidia familia.
Hata hivyo anasema kati ya watoto wake mwenye mapenzi na kazi hiyo ni mtoto wake wa mwisho Millsent pekee.
“Huyu mdogo hata dada zake wakiumia amekuwa mstari wa mbele kuwasaidia, atawafunga vidonda na hata dawa kabla haijatumika lazima ataikagua kama ni salama au vinginevyo.”