Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muswada kila bodaboda kuwa na bima ya afya wanukia

62004 Pic+bodaboda

Mon, 10 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema tangu usafiri wa Bodaboda kuruhusiwa kubeba abiria, Serikali ya Tanzania imekuwa ikiingia gharama kubwa kutibu wagonjwa wa ajali huku asilimia kubwa wakitibiwa kwa fedha za umma.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Juni 10, 2019 na Waziri wa Afya, Mwendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipokuwa akipokea miguu bandia 600 kwa ajili ya wenye ulemavu iliyotolewa na taasisi ya BMVSS kutoka nchini India.

Amesema kabla usafiri huo haujarasimishwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) ilikuwa ikipokea majeruhi 200 hadi 300 kwa mwezi.

"Tangu bodaboda irasimishwe kupakia abiria wagonjwa wameongezeka na Takwimu zinaonyesha MOI inahudumia wagonjwa 500 hadi 600 wa ajali kwa mwezi na wengi wanakatika miguu.

"Nipo kwenye mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Ndani, tunataka kupeleka muswada ni lazima kila anayeendesha bodaboda moja ya masharti lazima uwe na bima ya afya hii itaweza kusaidia wengi kuepuka ulemavu unaoweza kuzuilika na kupunguza mzigo wa serikali," amesema Ummy Mwalimu.

Aidha Ummy ameagiza wadau wanaotaka kutoa misaada ya miguu kuonana na wataalamu ili kutoa vifaa saidizi vyenye kusaidia wenye ulemavu.

Pia Soma

"Msitoe miguu hovyo hovyo tunatakiwa kuwa makini na kutumia wataalamu, nitoe maelekezo kwa wadau lazima watu wapimwe ili wakipata viungo viwasaidie na si kutoa kiholela mnawazidishia ugonjwa watu," amesema.

Balozi wa India nchini Tanzania, Sandeep Arya amesema miguu hiyo bandia ina thamani ya Sh1 bilioni.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dk Respicious Boniface amesema bei halisi ya miguu bandia ni Sh1.5 milioni mpaka Sh3 milioni na kwamba India wametoa bure.

Chanzo: mwananchi.co.tz