Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muswada bima ya afya kwa wote mbioni

Bima Muswada bima ya afya kwa wote mbioni

Fri, 14 May 2021 Chanzo: ippmedia.com

Akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia katika mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Naibu Waziri, Dk. Godwin Molel, alisema wengi walizungumzia bima ya afya kama kikwazo katika kupata huduma bora.

“Wakati wa kuleta muswada wa bima ya afya kwa wote tutahakikisha kuna kipengele kinachoruhusu sekta binafsi kushiriki kwenye bima,” alisema na kuongeza:

“Tumezingatia kabla ya kuleta bima ya afya kwa wote bungeni wananchi washirikishwe, wadau wote kuanzia wananchi ambao itawagusa kabla ya muswada kuja bungeni, tunaamini nanyi (wabunge) mtaweka mchango ili kuondoa matatizo yaliyopo kwenye bima ya afya iliyopo sasa,” alisema.

Aidha, Waziri huyo alikiri kuwapo kwa upungufu wa dawa na kusababisha wananchi wanaotumia bima ya afya kuhangaika na kutoona thamani ya kadi, huku baadhi ya maeneo wakisafiri umbali mrefu kufuata dawa katika maduka kwa kutumia nauli ya Sh. 10,000 kufuata dawa ya Sh. 3,000.

Naye Waziri wa Afya, Dk. Doroth Gwajima, alisema wameandaa utaratibu wa kuwa na wahudumu maalum wa wazee ambao watavaa fulana zilizoandikwa “Nakupenda Sana Mzee” ambao watawajibika moja kwa moja kwa kundi hilo.

Wakichangia mjadala huo, kilio cha ukosefu wa dawa, matibabu bure kwa wazee, wajawazito na watoto kilitawala, huku wakitaka hatua kuchukuliwa kuokoa maisha ya wananchi.

Watunga sheria hao walisema ukosefu wa wahudumu wa afya na wataalamu mbalimbali ni tatizo kubwa nchini, huku hakuna motisha kwa wafanyakazi.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Regina Qwaray, alisema huduma ya mama na mtoto ni bure, lakini maeneo mengi bila fedha hawapati huduma, huku wengine wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita 70.

Alisema huduma ya matibabu bure kwa wazee ni tatizo kubwa kiasi cha wengi kuteseka na kwamba ni muhimu kuchukua hatua kwa kuwa kila mmoja ni mzee mtarajiwa.

Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa (CCM), George Malima, alisema kutokana na ukosefu wa dawa wapo wauzaji wa maduka binafsi wanauza zilizopitwa na wakati jambo ambalo ni hatari kwa afya za watumiaji na kutaka serikali kufanya uchunguzi wa kina.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Martha Mariki, alisema mkoa wa Katavi kuna upungufu wa watumishi ni asilimia 72 waliopo ni asilimia 28, upungufu wa vifaa tiba ni asilimia 60 vilivyopo ni asilimia 40.

Aidha, alisema huduma ya damu kwa wajawazito ni tatizo kubwa kwa kuwa wanatakiwa kulipia na wanapoleta ndugu wa kuwachangia wanatakiwa kununua mifuko ya kuhifadhia Sh. 16,000.

Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Hawa Mwaifunga, alisema katika Hospitali ya Tabora wajawazito wanatozwa Sh. 50,000 kujifungua mtoto wa kiume na Sh. 40,000 mtoto wa kike.

Mbunge wa Jimbo la Tarime (CCM), Michael Kiambati, alisema kilio kikubwa cha wananchi wake ni ukosefu wa dawa kwa kuwa ni kawaida kwenda hospitali, kituo cha afya na zahanati na kukosa dawa.

Alisema maeneo mengi hakuna zahanati kiasi cha wajawazito wengi kupoteza maisha na kujifungulia njiani, huku hospitali pekee ya Bomani ikielemewa kwa wagonjwa na haina madaktari na wahudumu wa afya wa kutosha.

Alisema kutokana na upungufu wa watumishi wagonjwa wanaojiweza wanalazimika kufanya usafi kabla ya kupata huduma, jambo ambalo siyo sahihi.

Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini (CCM), Maimuna Mtanda, alisema wazee, wajawazito na watoto wanateseka kwa kukosa huduma sahihi, licha ya kuahidiwa huduma bure za afya.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Bahati Ndingo, alisema sera ya wazee ya mwaka 2013 haina sheria na kwamba ni muhimu serikali ikaeleza lini itaileta ili wapate huduma bila usumbufu.

Chanzo: ippmedia.com