Madaktari bingwa wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imetoa shanga ya plastiki iliyokuwa imekwama katika pafu la kulia la mtoto mwenye umri wa miaka mitano.
Akizungumza leo Januari 16, 2024 Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Kifua Mapafu na Mfumo wa Upumuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Mwanaada Kilima amesema shanga hiyo iliingia kwenye pafu baada ya kumpalia mtoto alipokuwa akiichezea mdomoni takribani mwezi mmoja uliopita.
Dk Kilima amesema mtoto huyo alitaabika tangu wakati huo kwa kikohozi na kupumua kwa shida huku njia mbalimbali zikitumika kujaribu kuitoa na kugonga mwamba, ndipo wataalamu wa mapafu walipofanikiwa kuitoa bila madhara yoyote.
“Tulitumia mpira laini wenye kamera ya video ya mapafu (Flexible bronchoscope) na kifaa cha kukamatia (foreign body basket) na kufanikiwa kuitoa hivyo kumwepusha na upasuaji mkubwa ambao ungesababisha ama kutoa pafu au sehemu ya pafu” amesema Dk Kilima.
Nae, Dk Ramadhan Hamis, Bingwa wa Upasuaji wa Kifua na Moyo ndiye aliyeoongoza jopo hilo amesema wazazi na wazazi wanapaswa kufuatilia michezo ya watoto kwa karibu zaidi na kuwazuia kuweka vitu mdomoni, puani pamoja na maskioni ili kuwaepusha na madhara mbalimbali ikiwemo madhara ya kudumu na kifo.