Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili yataka utafiti uhusiano tiba asili na hospitali

200398e84bdf6f77fc974f33b15d9fed.jpeg Muhimbili yataka utafiti uhusiano tiba asili na hospitali

Thu, 18 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WANASAYANSI nchini wametakiwa kufanya utafiti zaidi wa matokeo ya matumizi ya tiba asili na uhusiano wake na tiba ya hospitali ili kutoa majawabu sahihi kwa wananchi kuhusu usahihi wa tiba hizo mbili ili kuepusha madhara.

Aidha, wametakiwa kutafiti zaidi tiba mvuke kutokana na ukweli kwamba, wananchi wamekuwa wakichanganya majani ya aina nyingi katika kujifukiza kiholela huku wataalamu wakigundua kuwa, mvuke wa maji pekee ni sahihi kwa tiba hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru, alitoa mwito huo juzi wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa wataalamu wa afya katika hospitali hiyo Tawi la Mloganzila na baadaye kuzungumza na HabariLEO.

Mkutano huo ulijadili masuala mbalimbali yakiwemo mafanikio, changamoto na hatua zaidi za kuchukua kukabiliana na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19), magonjwa ya mfumo wa upumuaji na matumizi ya tiba asili na tiba mvuke katika kukabiliana nayo.

Profesa Museru alisema pamoja na hatua za serikali baada ya Covid-19 kuingia nchini mwaka jana na kudhibitiwa, wanasayansi wa ndani wanapaswa kutafiti kuhusu ugonjwa huo na mengine ya milipuko na matumizi ya tiba asili ili kutoa majibu sahihi kwa wananchi kuhusu ipi ni tiba sahihi na ipi siyo.

"Tufanye utafiti wa kutosha kuhusu hizi tiba za asili, zamani miaka na miaka tumetibiwa hivyo. Tunapoambiwa zinasaidia ama la, nani wa kutoa majibu kwa wananchi.”

“Mfano, kujifukiza kwa kuchanganya dawa na majani mengi kunaleta shida, tunaambiwa tutumie maji tu yanatosha. Ni sisi wanasayansi wa kutoa majibu haya," alisema.

Profesa Museru alitoa mfano kuwa ulifanyika mkutano wa kuchambua machapisho 2,000 ya utafiti kuhusu Covid-19, lakini cha kusitikitisha machapisho 60 pekee yalitoka nchi tatu za Afrika ambazo ni Nigeria, Misri na Afrika Kusini na yalichapishwa na watu wasioishi Afrika.

Alisema kutokana na hazina kubwa ya tiba asili zilizopo Afrika na Tanzania ikiwemo, anatamani siku moja utafiti wa wanasayansi nchini ugundue dawa ya kumaliza kabisa Covid-19 na kuisambaza ulimwengu mzima.

Juzi katika mkutano huo, wataalamu wa afya wakiwemo madaktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji katika MNH Mloganzila, walisema tiba ya kujifukiza maji yahachanganywi na kitu chochote kwani kuchanganya kunasababisha sumu na magonjwa ya kudumu kwa mtumiaji.

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani na Kitengo cha Uangalizi Maalumu (ICU) na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Mapafu, katika Hospitali ya Muhimbili, Tawi la Mloganzila, Dk Mwanaada Kilima, alisema walifanya utafiti mdogo na kubaini kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo kwa tatizo la upumuaji wanatumia tiba asili isivyo sahihi na kuhatarisha afya zaidi.

Dk Kilima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Magonjwa ya Ndani na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Covid 19 Mloganzila, alisema kwa upande wa tiba mvuke (kujifukiza), watu wengi wanaitumia isivyotakiwa kitaalamu kwani hawapaswi kuchanganya chochote katika maji ili kuepuka madhara ya kudumu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz