Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili yaokoa Tsh.bil 2/- kupandikiza uloto

Be500f1a328d3945a7d04bdb8b5906dc Muhimbili yaokoa Tsh.bil 2/- kupandikiza uloto

Tue, 8 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), imeokoa Sh bilioni 1.89 kwa kupandikiza uloto.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa MNH, Mkurugenzi wa tiba, Dk Hedwiga Swai alisema Dar es Salaam jana kuwa katika mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani wagonjwa 11 wamepata huduma hiyo.

“Muhimbili inaishukuru sana serikali. Imetupatia Sh bilioni 6.2 kwa ajili ya uboreshaji na ununuzi wa vifaa, ikiwemo kutengeneza sehemu ya kuandalia wagonjwa kwa ajili ya kupata dawa ya kupunguza makali ya kansa, sehemu ya kucheki seli na kununua mashine mbalimbali. Sasa tuna wagonjwa sita wanapandikizwa uloto hapo Mloganzila,” alisema Dk Swai.

Alisema gharama za upandikizaji ndani ya nchi ni Sh milioni 70 huku nje ya nchi ikiwa ni Sh milioni 250.

“Wagonjwa huwa wanahitaji damu nyingi, kwa mgonjwa mmoja anahitaji wachangiaji wa damu sita lakini kwa mashine mchangiaji mmoja anaweza kusaidia wagonjwa watatu kama ingekuwa haipo kwa wagonjwa watatu tungehitaji watu 18,” alisema Dk Swai na akaongeza: “Kwa ajili ya huduma hiyo kwa wagonjwa 11 serikali imetumia Sh milioni 770 lakini nje ingekuwa Sh bilioni 2.75,” alisema.

Dk Swai alisema Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika Mashariki na Kati na ya sita katika Bara la Afrika kupandikiza uloto. “Tumepata Sh bilioni 11.8 fedha za Covid-19 zimesaidia kununua vifaa mbalimbali vya ICU (vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu) na fahamu Muhimbili ina ICU sita.

Kuna huduma ya tiba, upasuaji, kinamama, watoto njiti, watoto wa kawaida na upandikizaji,” alisema Dk Swai.

Alisema mafanikio mengine ni ununuzi wa vifaa vinavyosaidia wagonjwa kama vile kuweka mifumo ya oksijeni, ventilator, isolation unit yenye vitanda sita na pia wametengeneza idara ya dharura na kwamba vifaa walivyoagiza vinaendelea kuwasili.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live