Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili yaleta mtambo kutambua maradhi

F2B10536 9D40 49FB A66A C325CB3A8494.jpeg Muhimbili yaleta mtambo kutambua maradhi

Sun, 25 Sep 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Kutokana na kukua kwa teknolojia ya matibabu, magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, sasa yataanza kuchunguzwa na kutibiwa papo hapo kwa kutumia teknolojia ya ‘Endoscopia’ (upasuaji wa matundu kwa kutumia kamera maalumu), baada ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufunga mashine hiyo maalum.

Mashine hiyo itakayosaidia utambuzi na tiba ya uvimbe kwenye utumbo na misuli ya tumbo pamoja na kuzuia damu kuvuja hasa kwa watoto, imenunuliwa kwa gharama ya Sh400 milioni na itakuwa ya kwanza kupatikana hapa nchini.

Hayo yamesemwa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Dk Hedwiga Swai wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kitaifa wa chama cha madaktari wa mfumo wa chakula na ini.

“Kupitia mkutano huu wataalamu wetu watakuwa wanajifunza namna ya kuitumia kutoka kwa wataalamu nje ya nchi na ni mashine ya kisasa ambayo tumeinunua kwa gharama ya Sh400 milioni inapatikana Muhimbili pekee,” alisema Dk Swai.

Hata hivyo, Dk Swai alisema licha ya uwepo wa mashine hizo, bado nchi haina wataalamu wa kufanya matengenezo ya mashine pindi zinapoharibika, hivyo juhudi za ziada zinapaswa kufanya ili kutengeneza wataalamu wa mashine na kuzuia gharama kubwa za matengenezo.

Rais wa chama cha madaktari wabobezi wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini (TAGES) Dk Elwaldo Komba alisema kabla ya ujio wa mashine hiyo, kulikuwa na ugumu katika uchunguzi na tiba.

“Kutokana na kukosekana kwa vifaa ilikuwa ngumu katika utambuzi. Mfano mtu anashindwa kumeza chakula unataka kujua kuna nini ili kutambua kwenye koo kuna saratani au njia imekua nyembamba, zamani tulikuwa tunatumia XRay.

“Tunampa mgonjwa ujiuji fulani anameza kisha tunafanya XRay kuona tatizo, lakini hiyo ni njia ngumu hata kama ukigundua pameziba, hauwezi kwenda pale sababu hakuna vifaa wakati mwingine walikuwa wanagundua matatizo lakini hauwezi kutibu,” alisema.

Alisema kupitia ‘endoscopia’ mtaalamu anaweza kugundua tatizo kwa kuona moja kwa moja na ataweza kutibu.

‘‘Kama koo limeziba anashindwa kumeza chakula, unaweka kifaa fulani kinaitwa ‘stant’ ni kama wavu fulani ukipachika sehemu iliyoziba ule wavu unafunguka njia inakua wazi imesaidia watu wengi,’’ alisema.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz