Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili yakaza uzi hadhari ya corona

8bffe65e0117aea0fd4b6cb6f34d2925 Muhimbili yakaza uzi hadhari ya corona

Wed, 23 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) kuanzia leo imeweka utaratibu wa kujikinga na ugonjwa wa virusi vya corona ambako watu wote wanaokwenda hospitalini hapo wanatakiwa wavae barakoa huku pia idadi ya wasindikizaji wa mgonjwa na wale wanaokwenda kuangalia wagonjwa ikipunguzwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa hospitali hiyo, Aminiel Eligaesha, utaratibu huo unaanza rasmi leo na utawahusu watu wote wakiwemo watoa huduma.

“Mtakumbuka serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeziagiza taasisi mbalimbali kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya corona na uwezekano wa kutokea wimbi la tatu la ugonjwa huo, na sisi tunaanza utekelezaji kesho (leo),” alisema Eligaesha.

“Wafanyakazi wote na wanafunzi kuanzia sasa wanapaswa kuvaa barakoa wakati wote wakiwa mazingira ya kazi, hakuna mfanyakazi atakayeruhusiwa kutoa huduma kama hana barakoa,” aliongeza Eligaesha na kubainisha hilo pia litawahusu wanaokwenda Hospitali ya Mloganzila.

Kuhusu kuepusha msongamano hospitalini hapo, alisema hospitali hiyo ina msongamano wa watu na hivyo mgonjwa anayekwenda kliniki ataruhusiwa kuwa na msindikizaji mmoja tu na kwa wagonjwa waliolazwa ndugu watano tu ndio wataruhusiwa kumuona na sio zaidi kwa siku moja.

Akifafanua hilo, alisema kwa wagonjwa waliolazwa, ndugu wawili wataruhusiwa kumuona mgonjwa wao asubuhi, mchana ni ndugu mmoja tu na jioni ni ndugu wawili tu. Aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi hizo ili kuongeza tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz