Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili yafanikiwa kumbadilisha damu mjamzito mwenye selimundu

4af31784607bdb33fba4bee5c63904b2 Muhimbili yafanikiwa kumbadilisha damu mjamzito mwenye selimundu

Sun, 19 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa mara ya kwanza imembadilishia chembe nyekundu za damu mjamzito mwenye ugonjwa wa selimundu.

Mwanamke huyo kwa sasa ana ujauzito wa miezi mitano huku akiwa amepoteza nyingine mbili kutokana na watoto kufariki kabla ya kufikia muda. Ubadilishaji huo wa damu umefanyika ikiwa ni baada ya hivi karibuni serikali kununua mashine mbili zenye thamani ya Sh milioni 245 ambazo zinatumika kutoa huduma ya upandikizaji uloto na huduma nyingine.

Akizungumza juzi Dar es Salaam, Daktari Bingwa wa magonjwa ya damu katika hospitali hiyo, Dk Yonaz Mbonea, alisema MNH imefanikiwa kubadilisha chembe nyekundu za damu kwa mjamzito mwenye selimundu ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika kwa tiba hiyo nchini.

“Kwa mjamzito kama huyu tutaendelea kumbadilishia chembe za damu nyekundu hadi atakapojifungua,” alisema Dk Mbonea na kuongeza kuwa awali matibabu ya kumbadilisha mgonjwa chembe nyekundu za damu ilikuwa ikifanyika kwa njia ya kawaida kabla ya kupata mashine hizo.

Alisema selimundu ni ugonjwa wa kurithi na mwathirika wa ugonjwa anakuwa amerithi vinasaba vya ugonjwa kutoka kwa wazazi wote wawili.

Mbonea alisema chembe nyekundu za damu ni kama kibebeo cha haemoglobini (wekundu wa damu) ambayo husafirisha hewa safi ya Oksijeni mwilini.

Alisema kasoro za chembe nyekundu za damu ni tatizo ambalo huathiri hali ya ujauzito na kuharibu mimba changa, kujifungua mtoto mfu, kujifungua kabla ya wakati na kujifungua mtoto mwenye uzito pungufu.

Mbonea alisema ugonjwa huo husababisha upungufu wa damu wa kudumu unaoambatana na njano ya macho, kutokana na kuvunjwavunjwa kwa kasi chembe nyekundu za damu.

Aliwasihi wajawazito wenye ugonjwa huo kuwahi kuhudumiwa na kuwa chini ya ufuatiliaji wa madaktari wa uzazi na damu, pia ni muhimu watu kujenga mazoea ya kupima afya na hasa kupima ili kujua hali ya kuwa na vinasaba vya ugonjwa huo.

Kwa upande wake, mjamzito aliyepata huduma hiyo, Esta Gabriella (25), alisema imemsaidia kwa sababu mwanzoni alikuwa na maumivu makali yaliyotishia uhai wake.

“Kiukweli hii huduma imeniokoa, nilikuwa na maumivu makali lakini kwa sasa niko kama tu yeyote wa kawaida sio mgonjwa tena,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz