Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili yaeleza mafaniko upasuaji pacha walioungana

19427 Pic+pacha TanzaniaWeb

Thu, 27 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanikiwa kufanya upasuaji wa  kuwatenganisha pacha walioungana waliozaliwa kijiji cha Vigwaza mkoani Pwani.

Upasuaji huo ulifanyika Septemba 22, 2018 ukishirikisha jopo la madaktari bingwa 10 wa upasuaji wa watoto.

Pacha hao ambao wote ni wavulana wamezaliwa Julai 12, 2018 kwa njia ya kawaida wakati mama yao akiwa njiani kuelekea hospitali.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Septemba 26, 2018 mkurugenzi mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru amesema sababu mojawapo ya mafanikio hayo ni uwekezaji katika huduma ya upasuaji.

Amesema tofauti na zamani, kwa sasa miundo mbinu ya upasuaji imeboreshwa hivyo hakuna haja ya kwenda nje ya nchi kufanya upasuaji unaoweza kufanywa nchini.

“Serikali imeboresha huduma hii ya upasuaji kwa watoto ili kupunguza gharama zisizo za lazima za kwenda nje ya nchi," amesema.

Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto,  Dk Petronia Ngiloi amesema watoto hao waliungana sehemu ya tumbo.

"Watoto hawa hawakuungana sana kitu ambacho walichangia ni maini hivyo tumefanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa tunaweza kuwatenganisha hapahapa nchini,"amesema.

Kwa upande wake mama mzazi wa watoto hao ambao bado hawajapewa majina,  Ester Simoni ameishukuru Serikali kwa hatua hiyo.

Nimefurahi kuwaona watoto wangu wametenganishwa nilikuwa najiuliza nitawalea vipi wakiwa wameungana," amesema Ester.

Watoto hao wenye umri wa miezi miwili wanaendelea na matibabu katika hospitali hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz