Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili yaanza upandikizaji mimba, ugumba ukiongezeka Tanzania

Sperm Ivf Muhimbili yaanza upandikizaji mimba, ugumba ukiongezeka Tanzania

Thu, 12 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Huduma ya upandikizaji mimba Intra–Vitro Fertilization (IVF) iliyoanza miezi michache iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, inatarajiwa kuzinduliwa rasmi kesho Alhamisi, Septemba 12, 2024 na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Phillip Mpango.

Gharama za upandikizaji ndiyo hasa kitendawili cha huduma hii, inayotarajiwa kwa wagonjwa watakaohitaji huduma hiyo yenye uhitaji mkubwa.

Wakati wa maandalizi ya huduma hiyo yanaanza mwaka 2019, kitengo hicho kilitaja kati ya Sh2 milioni mpaka Sh10 milioni, kuwa huenda ikawa ndiyo gharama kwa IVF.

Mpaka kufikia mwaka 2019 zaidi ya wanandoa 1,200 walikuwa wakisubiri huduma hiyo, baada ya Serikali kupeleka wataalamu nje ya nchi na kuanza rasmi maandalizi ya ujenzi wa jengo, vifaa na wataalamu.

Hata hivyo, changamoto ya ugumba imezidi kuongezeka nchini, baada ya Wizara ya Afya Agosti 2024, kutoa takwimu mpya zilizoonyesha wanawake 3,810 kutoka halmashauri zote nchini walijitokeza wakihitaji usaidizi wa kupata watoto.

Agosti 7, 2024 aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitoa ripoti ya utoaji wa huduma za kibingwa kwenye hospitali 184 ngazi ya halmashauri, iliyofanyika Mei mpaka Julai 2024.

Katika ripoti hiyo, jumla ya wagonjwa 70,000 waliopimwa afya, 18,044 walionwa na madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, ambako matatizo ya ugumba yaliongoza.

Alisema wagonjwa 3,810 sawa na asilimia 21 walikutwa na changamoto ya ugumba, kujifungua 2,529 sawa na asilimia 14 na tatizo la kutokwa na damu nyingi ukeni isivyo kawaida wagonjwa 2,108, sawa na asilimia 12.

"Hili nalo tunalitafakari kama tunakutana na wagonjwa wa ugumba wengi tunaliangalia, inabidi tulitafakari zaidi na hii ni changamoto kwa Watanzania wengi, ambao wamekuwa wakishindwa kupata matibabu kutokana na gharama kuwa kubwa," alisema Waziri Ummy.

Alipoulizwa kuhusu mchakato wa upandikizaji mimba katika Hospitali ya Taifa muhimbili na Bnejamin Mkapa wakati huo, Ummy alisema:

“Tumeshakamilisha kituo cha upandikizaji mimba, nilitaarifiwa kuhusu uzinduzi kwa upande wa Muhimbili ambao tayari wameshaanza kuwahudumia wagonjwa tayari. Kuna mawili matatu ya kukamilisha.

"Changamoto iliyoonekana ni gharama za sekta binafsi zinaleta changamoto na suala hili linawafanya wanawake wengi wanapitia unyanyapaa na ni sehemu ya haki ya mwanamke na mwanaume kupata huduma.

Kwa sasa tunafanya uchambuzi wa gharama ikiwezekana tuzipunguze kwa asilimia kubwa,” alisema, Ummy. Kwa sasa Waziri wa Afya ni Jenista Mhagama.

Akizungumza hivi karibuni katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mkuu wa Kitengo cha Upandikizaji Mimba Muhimbili, Dk Matilda Ngarina alisema Muhimbili kwa sasa wapo kwenye mkakati, wameanza kundi la kwanza la wagonjwa kwa kuwa upandikizaji hauwezi kufanyika kwa mtu mmoja.

“Lazima mwenza wake aje na kama nilivyosema, nusu inatoka kwa baba na nusu kwa mama, hatutaweza kuendelea na anayekuja peke yake.”

Alisema wanafanya hivyo ili kujua pia shida iko wapi. “Mara nyingi mwanamke anaweza akaja peke yake kwa maana mara nyingi wanawake ndiyo huwa tunaona hatuzai, ukishamwelewesha, mwanamume anakuja kwa shingo upande.

“Tunafanya uchunguzi na wakati wote huwa tunahangaika na kinamama, kumbe shida ipo kwa baba na mara nyingi tunagundua ni tatizo linalotibika kwa dawa pekee, anapata mtoto kwa njia ya kawaida.”

Alisema katika uhalisia wanaume kote duniani hawapendi kuonekana wana shida ya uzazi.

Kwa mujibu wa Dk Ngarina, kwa wanaume anaohitaji kujua tabia za mbegu zao wanapata nafasi kufanyiwa vipimo.

“Yeyote anayekuja kufanya kipimo anapata majibu, upo hapa tunakwambia mbegu zako zote zinatembea kutafuta yai,, hazina shida, mwingine tunamwambia pole hakuna mbegu kabisa.

“Wanakuja wengi huwataki kusema kwa nini wanapima mbegu zao, lakini unamsoma kwamba amegundua kuna shida anaomba kupima mbegu zake, tunawapima na kuwapatia majibu."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live