Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili wataja sababu tatizo la meno

F6433ebbd930114c75b841e471b2daa7.jpeg Muhimbili wataja sababu tatizo la meno

Fri, 2 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KUTOZINGATIA taratibu za usafi wa kinywa ni miongoni mwa sababu za tatizo la kulegea, kutoboka na kuoza kwa meno linalowakabili watoto na watu wazima katika jamii.

Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kimethibitisha kupitia elimu inayotolewa kwa wananchi wanaofika katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam.

Mtaalamu wa meno kutoka Muhas Dk Evarist Wilson anayetoa elimu katika banda la chuo hicho, alisema asilimia kubwa ya matatizo ya meno yanayowakabili watoto na watu wazima yanasababishwa na kutosafisha kinywa vizuri.

Alisema kuoza na kutoboka kwa meno kunasababishwa pia na matumizi ya sukari iliyosindikwa inayopatikana katika vyakula mbalimbalizikiwamo chokuleti, pipi, biskuti na soda.

“Sukari iliyosindikwa ambayo hupatikana katika vyakula vingi ndio chanzo cha meno kutoboka, kulegea pamoja na kuoza kutokana na matumizi ya sukari hiyo. Hili hutokea kwa watoto pamoja na watu wazima wanaotumia vyakula vya aina hiyo kwa wingi,” alisema Dk Wilson.

Mmoja wa wauguzi kutoka Muhas, Linus Mwelinde, alisema ili kuepuka madhara hayo yanayosababishwa na matumizi ya sukari zilizosindikwa, wananchi wanapaswa kuzingatia hatua mbalimbali za kusafisha kinywa ili kuondoa kabisa mabaki ya vyakula hivyo katika meno.

“Kuna hatua nne za kufuata zinazoweka kukinga meno dhidi ya matatizo yanayosababishwa na ulaji wa sukari zilizosindikwa hatua hizo zitafuatwa kikamilifu, kila mtu atabaki na meno yenye afya,” alisema Mwelinde.

Alisema wakati wa kusafisha kinywa watu wote wanapaswa kuanza na fizi za ndani kwa meno yote kabla ya kuja katika hatua ya pili ambayo ni katikati ya meno hasa ya kutafunia chakula.

Alisema hatua ya tatu ni kusafisha sehemu ya nje ya meno na fizi zake na hatua ya mwisho ni kusafisha sehemu ya juu ya ulimi.

Alisema kupitia hatua hizo, meno muda wote yatasalia masafi muda wote na kuepusha hatari ya kuoza au kutoboka.

Alisema kwa taratibu za kiafya inatakiwa kila mtu kusafisha kinywa kila baada ya kula pamoja na asubuhi baada ya kuamka.

Alisema watu wanafanya makosa ya kusukutua baada ya kusafisha kinywa kwa sababu wanaondoa dawa ambayo hulinda meno.

Chanzo: www.habarileo.co.tz