Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili wapokea mil 100/- kutibu saratani watoto

1a4da55fb6f0bb27e317777399b621cb.png Muhimbili wapokea mil 100/- kutibu saratani watoto

Fri, 6 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) iliyopo Dar es Salaam, imepokea Sh milioni 100 kusaidia zaidi ya watoto 2,000 wanaougua saratani na kutibiwa hapo.

Fedha hizo zilitolewa na Taasisi ya Mo Dewji Foundation.

Msimamizi wa watoto hao, Lilian Ngetabula, alilieleza habariLEO kuwa, idadi ya watoto wanaotibiwa saratani inaongezeka na kwamba, mwaka jana wagonjwa wapya 700 walifika kutibiwa ikilinganishwa na 600 mwaka 2019.

Wakati akipokea mfano wa hundi ya fedha hizo, Mkurugenzi wa Tiba katika MNH, Dk Hedwiga Swai, alihimiza wazazi wenye watoto wanaougua saratani kuwapeleka hospitalini hapo kwa kuwa ugonjwa huo unatibika kama wakiwahishwa.

"Jumla ya watoto 600 wanapatiwa matibabu ya kulazwa huku wengine wagonjwa 1,400 wamekuwa wakipatiwa matibabu ya nje kwa maana ya kuja na kuondoka," alisema Swai na kubainisha kuwa, gharama za kumtibu mtoto saratani ni Sh milioni 22 kwa mwaka, lakini katika hospitali hiyo hutolewa bure.

"Licha ya matibabu hayo kuwa ghali, MNH wamekuwa wakitoa matibabu hayo bure wakisaidiwa na taasisi ya Mo Dewji ambayo imekuwa ikitoa msaada wa kifedha kila mwaka," alisema Swai.

Alisema tiba ya saratani MNH imeokoa maisha ya asilimia 50 ya watoto ambao maisha yao yalikuwa hatarini.

Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya Tumaini la Maisha inayojihusisha na utoaji wa matibabu kwa wagonjwa wa saratani MHN, Gerald Mongella, aliwashukuru Mo Dewji kwa msaada waliotoa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz