Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili wapandikiza figo wagonjwa 68

C033a6eaff4f0c87ab0201038abd4661 Muhimbili wapandikiza figo wagonjwa 68

Mon, 7 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam imepandikiza figo kwa wagonjwa 68 tangu kuanza kwa huduma hiyo nchini mwaka 2017.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya figo, Onesmo Kisanga alisema hayo alipozungumza na HabariLEO jijini humo ikiwa ni maandalizi ya siku ya figo duniani itakayoadhimishwa Machi 11.

Dk Kisanga alisema takribani wagonjwa 110 hadi 120 hupata huduma ya kusafisha figo kila siku katika hospitali hiyo.

“Idadi ya wagonjwa inaongezeka tofauti na mwanzo, sababu ni mtindo mbaya wa maisha kwani magonjwa mengine kama kisukari na shikizo la damu yanaweza kusababisha tatizo la figo na sasa huduma za afya zimeboreshwa licha ya watu wanaofika hospitali kuongezeka,” alisema.

Aliongeza: “Hapa Muhimbili tuna mashine 42 za kusafisha figo ambayo kwa ukanda wa Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ni nyingi kuliko nchi nyingine.”

Dk Kisanga ambaye pia ni Rais wa Chama cha Madaktari wa Figo Tanzania alieleza kuwa utafiti ngazi ya jamii kaskazini mashariki mwa Tanzania unaonesha kuwa ugonjwa wa figo unaathri asilimia 6.7 ya watu kutokana na kutokuwa na uelewa wa ugonjwa huo.

Alisema ili kupunguza pengo kati ya watu wanaojua na wasiojua wataalamu wanaendelea kutoa elimu kupitia njia mbalimbali.

“Wiki hii tuna maandalizi ya siku ya figo duniani, inaadhimishwa kila alhamisi ya pili mwezi Machi na kaulimbiu ni ‘Afya kwa Wote.’ Tunataka watu wawe na elimu kusiwe na pengo katia ya watoa huduma na jamii.

Aliongeza: “Elimu itatolewa na wataalamu katika kila sehemu kama vile mitandaoni, kliniki na watu wawekwe tayari wahamasishwe kuwa na elimu ya figo.

Alibainisha kuwa Serikali imesomesha wataalmu na kuongeza vifaa ambapo hadi sasa kua madaktari bingwa 31 wa figo nchini.

“Kati ya hao wanawake ni 15 na wanaume ni 16 na pia Chuo kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) imeanza kutoa wauguzi, wataalamu wa mashine wa figo na sasa tunaendelea na elimu kupitia vyombo vya habari na mihadhara.

Dk Kisanga alisema mgonjwa ya figo yako ya aina mbili ambayo ni mshutuko wa figo na magonjwa sugu.

“Mshtuko unatokea kwa kinamama, kupata ajali, kuumwa na nyuki au nyoka. Hao wanaendelea vizuri wakipewa dawa lakini magonjwa sugu ni yale ya muda mrefu kama kisukari, shikizo la damu, kutumia dawa hovyo, dawa za kienyeji na mengine,” alifafanua.

Alishauri njia za kuepukana na tatizo hilo kuwa ni pamoja na kubadili muundo wa Maisha na kupima afya angalau mara moja kwa mwaka.

“Gharama za kusafisha figo ni Sh 200,000, hivyo nashauri kuwa na tabia ya kujiunga na bima ya afya, kupima afya angalau kwa mwaka mara moja, kufanya mazoezi na kutumia lishe inayofaa,” alishauri Dk Kisanga.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live