Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili wajengewa kituo cha umeme

14516 PIC+MHZ TanzaniaWeb

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imejengewa kituo kidogo cha umeme kitakachowapa umeme wa uhakika na kupunguza vifo vya wagonjwa vilivyokuwa vikisababishwa na kukatika kwa umeme.

Akizungumzia mradi huo uliofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (Jica) leo Agosti 29, Mkuu wa Idara ya Ufundi na Matengenezo - Muhimbili, Mhandisi Leonard Elizeus amesema kituo hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa Taasisi zilizo Muhimbili.

Amesema huko nyuma umeme ulikuwa ukikatika, huduma zilikuwa zinasimama, wauguzi wanashindwa kutoa huduma kwa sababu ya giza na kusababisha baadhi ya wagonjwa kupoteza maisha.

"Zamani umeme ulikuwa unakatika mara moja au mara mbili kwa wiki, tulikuwa tunatumia lita 2000 kuwasha jenereta kwa siku moja. Gharama zilikuwa kubwa lakini sasa tunapata umeme wa uhakika," amesema.

Elizeus amesema wakati mwingine mashine zinazotoa huduma zilikuwa zinasimama kama vile mashine za kufua mashuka. Amesema mambo yote yalikuwa yanachelewesha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

Kwa upande wake, Mhandisi Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Danstan Ndamugoba amesema kituo hicho kicho kina uwezo wa kuzalisha MW 12 wakati matumizi ya Muhimbili na taasisi zote nne ni MW 4.

Amesema Muhimbili wana ziada ya umeme ya MW 8 ambazo zitawawezesha kuendelea kujitanua na kuwa na uhakika wa umeme.

"Line iliyokuwa inatumika zamani ilikuwa inasambaza umeme katika maeneo mengine. Kwa hiyo umeme ulikuwa unakatika mara kwa mara hasa kutokana na shughuli za kibinadamu, mtu kagonga nguzo au mafuriko yakitokea," amesema.

Meneja wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) mkoa wa Ilala, Mhandisi Sotco Nombo amesema mradi kama huo unatekelezwa pia katika hospitali ya Mwananyamala, Ilala na Msasani ambayo kwa jumla imegharimu Sh88 bilioni ikiwa ni msaada kutoka shirika la Jica.

Chanzo: mwananchi.co.tz