Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili wafanya kweli tena, wapandikiza uloto

Bone Marrow Transplant  2.png Muhimbili wafanya kweli tena, wapandikiza uloto

Tue, 30 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MOJA ya huduma ghali duniani na ngumu inayohitaji ubobezi ya kupandikiza uloto kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na saratani za damu imezinduliwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Kwa uzinduzi huo Tanzania kwa mara nyingine tena inaandika historia kwenye utoaji huduma bobezi katika nchi zilizopo Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkurugenzi Mtendaji, Profesa Lawrence Museru alibainisha kuwa hospitali hiyo ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 48 kwa mwaka huku kila mwezi wakiwa na uwezo wa kupandikiza wanne.

Kwa uzinduzi huo Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kutoa huduma hiyo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati huku kwa Afrika ikiwa ya sita. Nchi nyingine zinazotoa huduma hiyo ni Afrika Kusini, Misri, Tunisia, Morocco na Nigeria.

Mkurugenzi huyo alisema hadi jana hospitali imeshapandikiza wagonjwa watano. Upandikizaji huo unajumuisha wagonjwa wenye selimundu, aplastatic anaemia na kadhalika.

Aidha, alisema kwamba gharama ya kufanyakazi hiyo Muhimbili ni Sh milioni 70 wakati kama mtu akitibiwa nje ya nchi angelazimika kulipia Sh milioni 250.

Alisema utoaji wa huduma ya uloto ni mafanikio ya uwekezaji wa Sh bilioni saba uliofanywa na serikali katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita zilizowezesha ununuzi wa vifaa na kusomesha wataalamu.

Akifafanua zaidi, Profesa Museru alisema: "Huduma hii inatolewa kupitia hospitali zetu mbili ambapo hapa Upanga ni shughuli za uchunguzi na kule Mloganzila ni kutokana na mgonjwa huyo kuhitaji mazingira maalumu. Mazingira ya Mloganzila yanaruhusu huduma hiyo kufanyika na kutunzwa kwa viwango stahiki."

Naye Daktari Bingwa wa magonjwa ya damu wa Muhimbili, Stella Rwezaula alibainisha kuwa madaktari wa hospitali hiyo wamejipanga kufanikisha utolewaji wa huduma hiyo kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia hatua mbalimbali anazotakiwa kupitia mgonjwa hadi kupandikizwa uloto.

Akizungumzia faida ya kufanyiwa matibabu hayo na kama mgonjwa aliyepatiwa matibabu ugonjwa unaweza kumrudia, Dk Stella alibainisha kuwa, inategemea na aina ya ugonjwa.

“Kuna aina ya saratani ya damu mgonjwa huwekwa kwenye matibabu ya kuhakikisha ugonjwa haurudi tena na kama ikitokea ukarudi basi maandalizi na upandikizaji hufanyika tena, ifahamike kuwa mgonjwa aliyefanyiwa upandikizaji huu huishi maisha ya kawaida kwa muda mrefu bila kupata adha ikilinganishwa na ambaye hajafanyiwa.”

Chanzo: www.habarileo.co.tz