Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili mbioni kupandikiza figo wenye magonjwa hatarishi

98809 Figo+pic Muhimbili mbioni kupandikiza figo wenye magonjwa hatarishi

Fri, 13 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili( MNH) imesema itaanza kupandikiza figo kwa wagonjwa wenye magonjwa hatarishi.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru amesema hayo leo Machi 12, 2020 wakati wa kongamano la siku ya figo duniani  lililohusisha viongozi wa dini.

"Kutokana na utoaji huduma hii kuimarika, MNH  itaanza kupandikiza figo kwa wagonjwa wenye vihatarishi  kiwango cha juu ikiwemo wagonjwa wenye maambukizi ya Ukimwi na homa ya ini. Wagonjwa waliowahi kupandikizwa figo lakini imeshindwa kufanya kazi vizuri, kuhitaji upandikizaji mara ya pili.”

“Katika hatua hii watu pia wasiokuwa na undugu nao watanufaika ikiwemo mke na mme na wale wenye matatizo ya shinikizo la damu" amesema.

Amesema upandikizwaji huo utaanza Aprili 2020 na kwamba wagonjwa wawili hadi watatu watafanyiwa upandikizwaji kwa siku, lengo likiwa ni kupandikiza figo wagonjwa 200 kwa mwaka.

Amebainisha kuwa inakadiriwa asilimia 10 ya watu duniani  wanasumbuliwa na ugonjwa wa figo na kila mwaka watu milioni 2.4 hufariki dunia.

Pia Soma

Advertisement
Amesema magonjwa ya figo yanashika nafasi ya sita miongoni mwa magonjwa yanayochangia idadi kubwa ya vifo duniani.

" Hapa nchini takwimu zilizotolewa na mwaka 2011 na  Shirika la Afya Duniani  zinaonesha kuwa Watanzania 4,300 hufariki kila mwaka kutokana na magonjwa ya figo, hii ni idadi kubwa hivyo kila mmoja wetu anao wajibu wa kukabiliana na tatizo hili,” amesema profesa huyo.

Amebainisha kuwa utafiti uliofanywa na MNH mwaka 2014 katika Mkoa wa Kilimanjaro, ulionyesha kuwa asilimia saba kati ya watu 100 waliochunguzwa walikuwa na wameathirika na ugonjwa sugu wa figo.

Amesema utafiti huo pia, ulibaini kuwepo kwa kiwango kidogo cha ufahamu kuhusu magonjwa ya figo, kwamba tangu kuanzishwa kwa huduma ya upandikizwaji wa figo nchini mwaka 2017 hadi sasa,  wagonjwa 56 wamepandikizwa figo Muhimbili.

“Upatikanaji wa huduma hii nchini umepunguza  gharama kubwa zilizokuwa zikigharamiwa na Serikali kupeleka wagonjwa nje ya nchi. Pia huduma zimesogezwa kwa watu wengi zaidi tofauti na hapo awali,” amesema.

Amesema upandikizaji figo MNH umeokoa Sh5 bilioni kwa maelezo kuwa  wagonjwa 56 wangepelekwa nje ya nchini, Serikali ingetumia Sh6.7 bilioni, “ lakini baada ya upandikizaji kufanyika nchini, Serikali imetumia Sh1.68 bilioni.  Kama mgonjwa mmoja wa figo atapelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kupandikizwa figo, gharama yake ni Sh30 milioni.”

Rais  wa Chama cha Wataalamu wa Figo nchini( Nesot), Dk Onesmo Kisanga amesema viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika kupeleka elimu kwa jamii ili iweze kujikinga na ugonjwa huo.

"Ili kuepuka magonjwa ya figo ni vizuri jamii ikazingatia kanuni bora za afya ikiwemo kufanya mazoezi, kuepuka matumizi ya pombe kali, matumizi ya dawa holela ya dawa kama mitishamba isiyothibitisha ubora, dawa za kupunguza maumivu na uvutaji wa sigara,” amesema  Dk Kisanga.

Richard Gikaro (37) ambaye amepandikizwa figo amesema alipata tatizo hilo mwaka 2013 na 2014 alianza matibabu MNH na sasa anaendelea vizuri.

" Moja ya changamoto ninayokabiliana nayo kwa sasa ni gharama ya dawa, natumia Sh2 milion kila mwezi kwa ajili ya kununulia dawa, hivyo naiomba Serikali iweze kuangalia namna gani ya kuboresha vifurushi vya bima ili wagonjwa wenye tatizo kama langu waweze kutibiwa kwa bima,” amesema.

 Mwenyekiti wa kamati ya amani Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa na makamu wake,  George Fupe ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, wamesema  watahakikisha wanaenda kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuchukua hatua ya kukabiliana na ugonjwa huo.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz