Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muhimbili kuanza kupandikiza mimba

Mimba D Watoto Muhimbili kuanza kupandikiza mimba

Fri, 11 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam inatarajia kuanza kupandikiza mimba (IVF) mwishoni mwa mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Mohamed Janabi amesema tayari mitambo ya huduma hiyo imeshafika nchini.

IVF ni upandikizaji wa kiinitete ndani ya kizazi baada ya uchavushaji wa mayai na mbegu kwenye maabara maalumu, kitendo hicho hufanyika kama mbadala wa hali ya kawaida ya utungaji wa mimba inapofanyika ndani ya mwili wa mwanamke katika mfuko wa uzazi.

“Mitambo tumeshaitoa bandarini wiki iliyopita, ni gharama kubwa mpaka ifungwe tukabidhiwe hivyo tuna imani kabla mwaka huu haujaisha huduma itaanza na itakuwa kwa gharama nafuu,” alisema Profesa Janabi wakati anazungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana.

Alisema baada ya muda mfupi kila kitu kuhusu mitambo ya huduma hiyo kitakuwa sawa kwa sababu jengo lilishaandaliwa siku nyingi.

“Jengo lilishaandaliwa ni kusubiri mitambo tu ifungwe na wataalamu waliokwishasoma wapo ingawa mwanzo tutafanya na wenzetu wenye utaalamu mkubwa ili kuwawezesha wataalamu wetu,” alisema Profesa Janabi.

Alisema kwa sasa ni ngumu kusema gharama za huduma hiyo lakini anawahakikishia wananchi itakuwa nafuu kwa kila anayehitaji kumudu.

Mara nyingi upandikizwaji mimba wa IVF huwa ni njia ya mwisho kwa wanandoa walioshindwa kupata mimba baada ya matibabu ya muda mrefu ambapo njia hii huleta matumaini kwao baada ya kukata tamaa ya kutafuta mtoto kwa muda mrefu.

Wanaoweza kutumia njia hiyo, ni wanawake ambao mirija yao imeziba, wanaume wenye manii/mbegu chache, utasa usioelezeka, baadhi ya wagonjwa wenye uvimbe kwenye ovari, viuvimbe vya vimeleo kuzunguka mfuko wa uzazi.

Wengine ni wanawake waliomaliza hedhi na wanahitaji mchango wa mayai, wanawake ambao wametolewa mfuko wa uzazi lakini ovari zao zimebaki, sababu za kijamii (kwa mfano mume anakwenda kwa ajili ya masomo au vita).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live