Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muda wa wagonjwa kupata tiba na vipimo JKCI kupungua

JKCI VIPIMOOOOOO Muda wa wagonjwa kupata tiba na vipimo JKCI kupungua

Mon, 19 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wagonjwa wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) watafanyiwa vipimo na matibabu kwa saa mbili badala ya saa nne wanayotumia sasa.

Hii ni baada ya jengo la wagonjwa linalojengwa na Serikàli kwa Sh3.6 bilioni ndani ya taasisi hiyo kukamilika kabla ya Agosti mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dk Peter Kisenge wakati wa ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe aliyetembelea Taasisi hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya kwa ajili ya wagonjwa wa moyo.

"Hospitali yetu kwa siku inahudumia wagonjwa 400 hadi 500 muda wanaotumia kupata huduma ni saa nne kwa hiyo jengo hili likikamilika nusu ya wagonjwa watahamishiwa kwenye jengo hili hivyo muda wa kuona wagonjwa utapungua kufikia saa mbili,"amesema.

Kutokana na umuhimu wa jengo hilo, Mkuu Wizara ya Afya, Dk Shekalaghe amemwagiza mkandarasi wa jengo hilo kufanya kazi usiku na mchana ili akamilishe kwa wakati.

"Jengo hili lilipaswa kukamilika Mei mwaka huu mpaka sasa bado mmeomba nyongeza ya miezi mitatu, nawaagiza mfanye kazi usiku na mchana hata kabla ya huo muda mlioomba mkamilishe ujenzi,” amesema.

Pia kwa uongozi wa taasisi hii wasisubiri jengo likamilike ndipo waanze kuweka vifaa, nataka jengo hili likikamilika vifaa vyote viwe vimewekwa na siyo kukamilika na kuanza kusubiri vifaa," amesema.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Sh3.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo na kinapaswa kukamilika kwa wakati ili wananchi wapatiwe huduma.

Mbali na hayo Dk Shekalaghe amemwagiza Mkurugenzi wa JKCI kuhakikisha, madaktari bingwa ndani ya taasisi hiyo wanawajengea uwezo wa kimatibabu wataalamu wa hospitali za rufaa mikoani, ili wagonjwa wanaofikishwa kwenye taasisi hiyo wawe ni wale kweli wanaohitaji huduma za kibingwa.

Kwa upande wake Mhandisi wa jengo hilo wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Baraka Kilungu amesema mpaka sasa jengo hilo ujenzi wake umefikia asilimia 71.

Amesema sababu ya kuchelewa kukamilisha jengo hilo, ni eneo ambalo jengo lilipaswa kujengwa kuwa na mitambo ya gesi hivyo muda mwingi kutumika katika kuondoa mitambo hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live