Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtu mzima anatakiwa kutumia chumvi kijiko kimoja

Chumvi Kijiko Kimoja Mtu mzima anatakiwa kutumia chumvi kijiko kimoja

Fri, 30 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa Shirikisho la Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza Tanzania, Profesa Andrew Swai amesema mtu mzima anatakiwa kutumia chumvi kijiko kimoja cha chai siku nzima kwenye vyakula vyote atakavyokula siku hiyo.

Profesa Swai amebainisha hayo jana Alhamisi Septemba 29, 2022 wakati akizungumza na kituo kimoja cha redio kuhusu ugonjwa wa moyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Moyo duniani inayoadhimishwa leo.

Amesema chumvi ndiyo chakula kinachosababisha magonjwa yasiyoambukiza kwa kiwango kikubwa, hivyo amewashauri watu kutumia kiwango kidogo cha chumvi sambamba na kufanya mazoezi ili kupunguza chumvi hiyo.

Profesa Swai amebainisha mtu mzima anatakiwa kutumia chumvi kijiko kimoja cha chai siku nzima kwenye vyakula vyote atakavyokula siku hiyo. Amesema chumvi inapenda maji kwa wingi, jambo linaloweza kusababisha shinikizo la damu.

“Mwilini, chumvi ikizidi inazuia maji yasitoke kwa sababu popote ilipo inang’ang’ania yale maji. Kazi ya figo ni kupunguza maji yaliyozidi mwilini, lakini ikiwa chumvi imezidi, maji yanabaki mwilini.

“Maji yakibaki mwilini, pressure (shinikizo la damu) inapanda, pressure ikipanda inaleta matatizo, ile mishipa inaweza ikapasuka,” amesema Profesa Swai ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala.

Amesisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi kama njia moja wapo ya kuondoa chumvi iliyozidi mwilini ili kumuweka mtu katika afya bora.

Profesa Swai amesema “chumvi ni chumvi, haijalishi umeipika au hujaipika, chumvi ni chumvi. Kinachoingia mwilini ni sodium na chloride yake, kwa hiyo itakuletea matatizo. Ni kama sukari, sukari ni sukari, iwe ni asali au sukari ya nini…sukari ni sukari.”

Kwa upande wa mafuta ya kula, Profesa Swai amesema mtu mmoja anatakiwa kula kiasi cha mafuta kisichozidi ujazo wa kidole gumba kwa siku.

“Tunatakiwa vyakula vyetu viwe na nyuzi nyuzi za kutosha. Hii inahusisha mboga za majani, aina zote za matunda lakini bila kukamua.

“Nyuzinyuzi zile ni muhimu kwa sababu yanasaidia sukari na mafuta yale mabaya yanatoka pamoja na nyuzinyuzi,” amesema Profesa Swai ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha ugonjwa wa kisukari.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live