Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtu mmoja kati ya saba hugundulika na Corona Afrika

Majestic Cell Corona E1584032867403 660x400.png Mtu mmoja kati ya saba hugundulika na Corona Afrika

Mon, 18 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Tathmini mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonyesha ni asilimia 14.2 tu sawa na mtu mmoja kati ya watu saba walioambukizwa Uviko-19 hugunduliwa barani Afrika.

Ripoti hiyo iliyotolewa Oktoba 14, imeeleza kuwa ili kubadili mwenendo huo na kuzuia maambukizi kusambaa, Ofisi ya Kanda (WHO ya Afrika) imetangaza mpango mpya wa kuongeza kasi ya upimaji Uviko-19 katika nchi nane.

Mpango huo unakusudia kufikia zaidi ya watu milioni 7 na vipimo vya haraka vya uchunguzi kwa mwaka ujao.

Uchambuzi wa WHO ulitumia kikokotoo cha Uviko-19 kilichotengenezwa na ‘Resolve to Save Lives’ ambayo inakadiria maambukizi kulingana na idadi ya visa na vifo na kiwango cha vifo vya maambukizi kilichowekwa kwa idadi ya watu.

Kikokotoo hicho kiligundua kuwa kufikia Oktoba 10, 2021 idadi ya jumla ya maambukizi ya Uviko-19 inakadiriwa kuwa milioni 59 barani Afrika, ambayo ni mara saba zaidi ya visa zaidi ya milioni 8 vilivyoripotiwa.

Hadi sasa, ugunduzi wa Uviko-19 barani Afrika umezingatia watu wanaoripoti katika vituo vya afya na dalili, pamoja na majibu ya vipimo vya wasafiri wa kimataifa.

Tangu kuanza kwa janga hilo mpaka kufikia Oktoba 10, zaidi ya vipimo milioni 70 vya Uviko-19 vimeripotiwa na nchi za Afrika, ambayo ni sehemu ya watu bilioni 1.3 wa bara hilo.

Kinyume chake, Marekani na karibu theluthi moja ya idadi ya watu, imeripotiwa kutumia vipimo milioni 550, wakati Uingereza imetumia milioni 280.

"Pamoja na upimaji mdogo, vipimo vingi hufanywa kwa watu walio na dalili, lakini maambukizi mengi yapo kwa watu wasio na dalili, kwa hiyo kile tunachokiona kinaweza kuwa ncha ya barafu.

Mpango huu wa jamii ni njia mpya ambayo inapaswa kusaidia kuongeza viwango vya ugunduzi, " alisema Dk Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa Kanda wa Afrika wa WHO.

Nchi zitakazoshiriki katika mpango huo ni Burundi, Cote d'Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guinea-Bissau, Msumbiji, Jamhuri ya Kongo, Senegal na Zambia. Ili kuanza utekelezaji, WHO imetoa Dola za Marekani milioni 1.8 kwa nchi nane.

Nchini Tanzania mpaka kufikia Oktoba 2, waliothibitika kuwa na maambukizi walikua watu 26,034, vifo 724 na waliochanja 885,579.

Wakati hali ya uchanjaji ikiongezeka, Mkurugenzi Mkaazi wa WHO Tanzania, Dk Tigest Ketsela Mengestu alisema kupungua kwa maambukizi kunatoa nafasi sasa kwa wengi kufanya maamuzi ya kuchanja ili kuongeza kinga miongoni mwa jamii.

“Matarajio ni kufikisha asilimia 60 ya waliochanja Tanzania ili kutengeneza kinga kamili kwa jamii. Hali ya uchanjaji inaimarika tunawapongeza Watanzania walioamua kuchukua hatua ya kuchanja pia tunaipongeza Serikali kuanzisha kampeni ambayo imezaa matunda,” alisema Dk Tigest.

Mtaalamu wa chanjo WHO, Dk William Mwengee alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 85 ya wanaopata maambukizi ya Uviko-19 hawaonyeshi dalili yoyote.

Mpaka sasa zaidi ya watu bilioni 6.5 duniani wameshachanja chanjo ya Uviko-19 na kwamba miongoni mwa nchi ambazo watu wake wamechanja kwa kiasi kikubwa (zaidi ya asilimia 60 ni pamoja na Uingereza, Marekani, Italia.

Hata hivyo hakuna nchi barani Afrika ambayo imefikia uchanjaji wa asilimia 60 ya raia wake.

Mtaalamu wa matibabu WHO, Dk Nemes Iriya alisema gharama za matibabu ya ugonjwa huo ni kubwa hivyo Watanzania wanatakiwa kujikinga ipasavyo kwa kupata chanjo.

Alisema mpaka sasa hakuna dawa iliyopatikana ambayo inatibu ugonjwa huo, “Mpaka sasa hatuna dawa ya uhakika na zilizopo ni chache ambazo zinatibu dalili kwa kupunguza makali ya Uviko-19 dawa ambazo bado ni ghali.”

Chanzo: mwananchidigital