Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto mwenye VVU asiambiwe hadi miaka 10  

F29e45ec029ab468094e1ca8f7c75bf5 Mtoto mwenye VVU asiambiwe hadi miaka 10  

Mon, 19 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MTOTO mdogo anayeishi na Virus Vya Ukimwi (VVU), asielezwe moja kwa moja tatizo linalomsumbua, bali aambiwe tu kwamba ana ‘mdudu mbaya’ mwilini mwake.

Hatua hiyo inasaidia pamoja na mambo mengine, kumjenga mtoto ipasavyo kisaikolojia ili utakapofika wakati wa kuuelezwa ukweli, aipokee na kuikubali hali hiyo, ambayo ndiyo atakayoishi nayo maishani mpaka tiba ya Ukimwi itakapopatikana.

Hata hivyo, asifikishe umri wa miaka 10 bila ya kujua kwamba sio ‘mdudu mbaya’ bali ni VVU, njia zinazoweza kuwa sababu ya yeye kuambukizwa na vilevile ni jinsi gani anaweza kuzuia maambukizi mapya kwake na kwa wengine.

Inasistizwa kwamba kuanzia miaka sita hadi 10 mtoto awe ameujua ukweli, si tu kujikinga au kukinga wengine na maambukizi bali mimba za utotoni.

Mgonjwa hatakua na uwezo wa kuambukiza wengine pale tu matokeo ya vipimo yasipoonesha wingi wa VVU mwilini mwake.

“Wingi wa virusi kwa lugha ya kitaalam tunaita ‘nakala’ (copy). Kama idadi ya nakala ni chini ya 50 mwilini, uwezekano wa kuambukiza ni mdogo,” anasema Daktari wa Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya VVU la AGPAHI, Ayoub Msalilwa.

Msalilwa anayasema hayo siku ya kliniki ya watoto wanaoishi na VVU hivi karibuni, katika kituo cha afya Makongoro wilayani Nyamagana, jijini Mwanza.

Anaelimisha zaidi kwamba kupungua kwa idadi ya nakala ni matokeo ya matumizi bora ya dawa za kufubaza virusi (ARVs).

Utaratibu wa kituo cha Afya Makongoro, chenye idadi ya watoto wanaoishi na VVU 46 (umri chini ya miaka 15) ni kwamba mtoto mwenye nakala zaidi ya 50 huhudhuria kliniki kila mwezi na wale wa chini ya idadi hiyo ni kila baada ya miezi mitatu.

“Maana yake ni kwamba kwa wenye nakala nyingi hupewa dawa za siku 30 tu na kupimwa kila mwezi wanapofuata dawa zingine, ambayo ndiyo siku ya kliniki yao. Wenye nakala ndogo hupewa dawa za siku 90,” anasema.

Inaelezwa pia kwamba Shirika hilo kwa kushirikiana na serikali hutoa mafunzo kwa watoa huduma ili kufuatilia kwa ukaribu matumizi ya ARVs kwa walengwa.

Huwafuata wagonjwa majumbani mwao ili kuchunguza pia kama kuna changamoto zingine wanazokumbana nazo, ikiwemo unyanyapaa unaoweza kuwakatisha tamaa ya kutumia dawa, kwa vile kutotumia dawa ipasavyo ni kuvipa nafasi virus kushambulia kinga za mwili na kumdhoofisha zaidi mgonjwa.

Kufuatilia hali ya lishe kwa watoto wanaoishi na VVU ni kazi pia ya watoa huduma ili kuhakikisha wanakula vizuri, hivyo kuzuia kinga za mwili kushuka kwani zikishuka huruhusu magonjwa nyemelezi yanayomuathiri zaidi mgonjwa.

Kwa wenye upungufu wa lishe Shirika limekuwa likitoa misaada ya chakula na huduma zingine muhimu.

“Kwa ufuatiliaji huo, watoto wa kituo hiki wamefubaza virusi kwa asilimia 98 na hivyo kuvuka lengo la kidunia la 95-95-95,” anasema.

Anafafanua kwamba lengo hilo maana yake ni kwamba ifikapo mwaka 2030 asilimia 95 ya wanaoishi na VVU wawe wamejua hali ya afya zao, asilimia 95 wameanza kutumia ARVs na asilimia 95 tayari wamefubaza VVU.

Akizungumzia nini hasa chanzo cha watoto hao kupata maabukizi, Dk Msalilwa anasema ni uchelewaji wa baadhi ya wajawazito kuanza kliniki, hivyo kukosa elimu na huduma zingine za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Wapo ambao wanaozembea kuanza au kutohudhuria kliniki kabisa katika kipindi chote cha ujauzito, wakati mama akiwahi kliniki hupimwa afya yake na akikutwa na maambukizi huataanza ARVs mapema na hivyo kupunguza uwezekano wa kumuambukiza mtoto wakati wa kujifungua.

Takiwmu zilionesha kwamba katika robo ya kwanza ya mwaka huu idadi ya wajawazito mkoa wa Mwanza ilikua 28,765 na kati yao 1,159 walikua wanaishi na VVU.

Kati ya wenye VVU, tisa walijifungua watoto wenye maambukizi na uchunguzi ulionesha ni mama waliochelewa kupata huduma za kliniki na wale waliojifungulia nyumbani.

Kawaida mjamzito anashauriwa kuhudhuria kliniki pindi tu anapojihisi kuwa mjamzito, ambayo ni wiki nane (baada ya kushika ujauzito).

Kwa mama aliyechelewa kuanza kliniki, akagundulika siku za mwishoni kwamba ana VVU, ndani ya saa sita baada ya kujifungua mtoto hupewa dawa maalumu ya kuzuia maambukizi (presumprive ARV).

Mtoto huendelea kupewa dawa hiyo kwa muda wa wiki 12 huku uchunguzi mwingine ukifanyika, na akifisha umri wa mwaka mmoja na nusu hupimwa rasmi ili kuhakikisha hali ya afya yake.

Mara nyingi kupimwa kabla ya umri huo imekua ni changamaoto kwani asilimia kubwa ya damu ya mtoto inakua bado imechanganyikana na ya mama yake, hatua inayohofiwa kutoa majibu yasiyo sahihi.

Katika jitihada zaidi za kuzuia maambukizi mapya AGPAHI imekua ikianzisha vituo/klabu za watoto wenye VVU katika vituo mbalimbali vya afya, ikiwemo Makongoro, kwa elimu endelevu juu ya ugonjwa huo.

Kwa mkoa wa Mwanza Shirika lina vituo zaidi ya 180 kwa ajili ya vijana na watoto wanaoishi na VVU.

Ni klabu za aina mbili kwa ajili ya watoto wa umri wa miaka 10 kushuka chini na wale wa miaka 11 hadi 18, ambao hukutana kwa mwezi mara moja kwa ajili ya elimu endelevu lakini pia kuchangamana na kubadilishana mawazo kwa namna tofauti, ikiwemo michezo mbalimbali.

Akizungumzia uchelewaji wa mama wajawazito kuhudhuria kliniki, Mkuu wa kitengo cha Tiba na Matumizi (CTC) katika kituo cha afya Makongoro, Bahati Mbaga anasema wachelewaji wapo lakini idadi inapungua takribani kila siku.

Anasema uwepo wa mradi wa ‘Boresha’ (2016- 2021) unao utekelezwa na AGPAHI kwa kushirikina na serikali katika vituo mbalimbali vya Afya umechangia kupunguza idadi ya wajawazito wachelewaji.

Anasema kwa sasa kituo kinaweza kupokea mjamzito mmoja tu kwa mwezi au baada ya miezi miwili hadi mitatu anayechelewa kuanza kliniki.

Mradi wa Boresha umesaidia kutoa elimu kwa umma pamoja na kumshawishi kila mwananchi anayeingia lango la hospitali kupima VVU hata kama ana shida nyingine.

“Uhimizaji wa kila mtu kujua afya yake ni sehemu pia itakayofanikisha nchi kufikia lengo la kidunia la 95-95-95. Kwa upande wa watoto, tulionao hapa ni 60 ambapo 46 ni wa chini ya miaka 15 na 14 ni zaidi ya hapo,” anasema.

Mbaga anasema uwepo wa klabu za watoto kituoni hapo umekua mojawapo ya vichocheo vya kufubaza virus hadi kuvuka lengo la kidunia.

“Na Shirika linawapatia posho za usafiri na linaandaa chakula kila wanapokutana pamoja na michezo mbalimbali, hali inayowashawishi wengi kuhudhuria. Wakikutana kipaumbele chetu ni elimu ya matumizi bora ya dawa ili kuzuia maambuki mapya,” anasema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz