Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto azaliwa bila ubongo

63a682a7d990a74b3dd0e62f1dde39ba Mtoto azaliwa bila ubongo

Wed, 30 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKAZI wa Kijiji cha Mlowo mkoani Songwe, Loveness Kweka (25), amejifungua mtoto wa kiume asiye na ubongo na mfupa wa juu wa kichwa. Mtoto huyo amezaliwa wiki iliyopita katika Hospitali Teule ya Mkoa wa Songwe mjini Vwawa.

Akizungumza na HabariLEO kwa simu, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Lukombodzo Lulandala alisema mtoto huyo alizaliwa akiwa hai na uzito wa kilogramu 2.5.

Dk Lulandala alisema mtoto huyo ni wa pili kwa Loveness na alijifungua kwa njia ya kawaida baada ya ujauzito kukamilisha miezi tisa.

“Mtoto licha ya hitilafu hizo alizo nazo za uumbaji, amezaliwa kwa njia ya kawaida akiwa hai akiwa na uzito wa kilo 2.5... Mtoto na mama yake waliendelea kuwa chini ya uangalizi wa wauguzi kwa zaidi ya saa 23 tangu alipozaliwa, lakini ndugu wa mwanamke wakisisitiza wamchukue wakamlee nyumbani…”

“Nilipowahoji walionesha hisia zao za kumtompenda mtoto walimchukua akiwa hai ila kwa sasa sina taarifa zake kama yuko hai au la,” alisema. Dk Lulandala alisema baada ya mimba kutungwa siku nane za mwanzo hitilafu za uumbaji zinaweza kujitokeza na kusababisha mtoto azaliwe akiwa hana ubongo au mgongo wazi hivyo hitilafu za uumbaji zisihusishwe na imani za kishirikina.

“Akiwa tumboni pamoja na hitilafu za uumbaji mtoto ataendelea kuishi bila matatizo kwa sababu kila kitu anategemea kupata kutoka kwa mama yake tumboni,” alisema.

Alitahadharisha kuwa mimba katika miezi mitatu ya mwanzo matumizi ya dawa bila ushauri wa daktari si salama kwa wajawazito.

Kwa mujibu wa Dk Lulandala, wanawake walio kwenye hatari ya kujifungua watoto wenye hitilafu za uumbaji ni pamoja na wanaosumbuliwa na magonjwa ya kisukari na wenye uzito mkubwa. Alishauri wanawake wanapokuwa wajawazito wahudhurie kliniki kwa uchunguzi wa kitabibu na ushauri badala ya kunywa miti shamba.

Dk Lulandala alisema, tatizo la watoto kuzaliwa bila ubongo na mfupa wa juu ya kichwa lipo kidunia na kwamba, kati ya vizazi 10,000 watoto 400 wanazaliwa wakiwa na hitilafu za uumbaji.

Alisema utafiti uliofanywa mwaka 2012/2013 ulionesha kuwa watoto 28 walizaliwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakiwa na hitilafu za uumbaji.

Chanzo: habarileo.co.tz