Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto aliyedondoka mtini akikata fimbo aeleza sababu ya kuomba kutibiwa nje

32847 Pic+mtoto Tanzania Web Photo

Sat, 22 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Moses Gabriel (14), mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Samora Machel mkoani Mbeya aliyevunjika uti wa mgongo miezi minane iliyopita ametaja sababu ya kuomba msaada wa kutibiwa nje ya nchi.

Moses anaomba kupatiwa matibabu nje ili aweze kupona haraka na kuendelea na masomo.

Mwanafunzi huyo ametaja sababu nyingine kuwa tangu Aprili 25 alipopata ajali hiyo amekuwa akilala kitandani na hawezi kukaa wala kutembea. Moses alivunjika uti wa mgongo baada ya kudondoka kutoka mtini alikotumwa na mwalimu wake wa hisabati kwenda kukata fimbo ambazo zilipaswa kutumika kuwaadhibu wanafunzi waliokuwa wamefeli somo hilo.

“Sina uwezo tena wa kuinuka, kutembea wala kwenda shuleni kwa sababu hata nikijisaidia haja zinakuja bila taarifa, naamini nikisaidiwa kama walivyosaidiwa watoto wa Lucky Vincent nitapona, naombeni msaada,” alisema Moses.

Watoto watatu walionusurika katika ajali ya gari lililowabeba wanafunzi wa Lucky Vincent iliyotokea Mei 6, 2017 walitibiwa nchini Marekani na kurejea wakiwa na afya njema. “Wenzangu walirudi wanatembea na mimi nina uhakika nikipelekwa huko nitarudi natembea, mama yangu hana uwezo wa kunipeleka huko ila kwa msaada wenu.”

Mbunge wa zamani wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ndiye aliyewasaidia wanafunzi wa Lucky Vincet kutibiwa nchini humo.

Hata hivyo, Moses alisema, “Siyo kwamba madaktari wangu hawafanyi kazi nzuri, hapana, sikuwa hivi. Ila natamani kupona haraka, utaalamu wa nje kama ule waliopatiwa wenzangu kulingana na hali yangu utanisaidia.”

Aliwashukuru Watanzania wanaoendelea kumchangia fedha kwa ajili ya matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili anakotibiwa kwa sasa.

Swaumu Sesemi, mama yake Moses alisema, “Mpaka hapa tulipofika ni kwa uwezo wa Mungu, kama alivyosema (mwanangu) tunaomba apelekwe huko nje anaweza kurejea kwenye hali yake ya kawaida na akaendelea na masomo.”

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mwita Waitara alipoitembelea familia hiyo alisema wameunda kamati kuchunguza tukio hilo.

Pia, Waitara alikabidhi Sh9 milioni kama mchango wao kwa ajili ya matibabu ya mwanafunzi huyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz